Watu watano mkoani Kagera wamefariki dunia katika matukio tofauti wakiwamo wanandoa wawili huku mwingine akiuawa kwa kuchinjwa shingo na sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kuchomwa moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema jana kuwa wanandoa Mkundwa Selestine (51) na mkewe Letisia Katawa (48) walikutwa wamefariki katika Kijiji cha Ngararambe Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo vifo vyao vikihusishwa na kukosa hewa ndani ya nyumba baada ya kuacha jiko la mkaa likiwaka.
Katika tukio jingine la Januari 19, lililotokea katika Kitongoji cha Nyakanyasi, Tarafa ya Kaisho Wilayani, Peter Ezekiel ( 27 ) alikutwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili chumbani kwake.
Kamanda Malimi alisema mbali ya Ezekiel kuchinjwa shingo, alikatwa kichwani na kuondolewa sehemu zake za siri na kisha mwili wake kupelekwa katika chumba kingine na kuchomwa moto na watu wasiojulikana. Alisema chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa.
Kamanda huyo alisema tukio jingine lilitokea Januari 21 katika Kitongoji cha Kyenguge Kata ya Katereteo, Bukoba. Katika tukio hilo, Rwegasira Godwine (29 ) alikutwa sebuleni nyumbani kwake akiwa amepigwa na kitu kizito kichwani na mwili wake kuchoma moto.
Alisema kabla ya tukio hilo ulitokea ugomvi kati ya marehemu na vijana wawili ambao ni aliwataja vijana wawili waliokuwa marafiki zake ambao alisema walihitilafiana kwa kutembea na mwanamke ambaye ana uhusiano wa kimapenzi na marehemu.
Kamanda huyo akielezea tukio jingine la mauaji lililotokea katika Kitongoji cha Kibamba, Kijiji cha Nyabugombe wilayani Biharamulo ambako Philbert Kinyana (37) mfugaji na mfanyabiashara wa nyama, mkazi wa Ngara mjini alipigwa risasi na watu wasiojulikana.
Na Shaaban Ndyamukama, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment