MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa kibali cha kufungua kesi ya
uwakilishi, kwa wanafunzi wanne, waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Joseph kwa madai ya kutokuwa na sifa za kudahiliwa kwenye vyuo
vikuu.
Jaji
Eliezer Feleshi alitoa kibali hicho baada ya wanafunzi hao kuwasilisha
maombi ya kibali cha kuwakilisha wenzao mahakamani pamoja na kusitisha
masomo wakati kesi ya msingi ikiendelea kusikilizwa.
Wanafunzi
hao, walisimamishwa masomo baada ya kutolewa amri ya Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako kwamba
kutokana na tatizo la ufundishaji wa Stashahada ya Elimu (Sayansi,
Hisabati na Teknolojia) wanafunzi wote wanatakiwa kurejea nyumbani.
Akiwasilisha
maombi ya wanafunzi hao, Wakili Emmanuel Muga aliomba wanafunzi 316
waliofukuzwa chuo, wapewe kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi pia
Mahakama itoe amri ya kusitisha masomo wakati wa usikilizwaji wa kesi.
Akitoa
uamuzi, Jaji Feleshi alisema Mahakama imekubali ombi hilo, isipokuwa la
kusimamishwa masomo wanafunzi wote na kufafanua kuwa “masomo
yataendelea kusimama kwa wanafunzi 316 waliosimamishwa”.
Aidha
alisema wanafunzi hao wanatakiwa kuwa na wawakilishi wanne tu, badala
ya 316, kwa sababu idadi yao ni kubwa. Baada ya uamuzi huo, Wakili Muga
aliwataja wanafunzi wanne watakaowawakilisha wenzao mahakamani hapo kuwa
ni Innocent Peter, Ramadhan Kipenya, Oswald Mwinuka na Faith Kyando.
Jaji
Feleshi alisema Mahakama imetoa kibali na itapanga tarehe ya
kusikilizwa kwa kesi baada ya walalamikaji hao kufungua kesi yao.
Katika
madai yao, wanafunzi hao wanadai fidia ya miaka mitatu waliyokaa chuoni
hapo dhidi ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) iliyowakilishwa na Wakili Rose
Lwita na Judith Misokia na Chuo cha Mtakatifu Joseph, kikiwakilishwa na
wakili Jeromah Msemwa.
0 comments:
Post a Comment