Wakati
Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mbeya ikiutaka uongozi wa Bunge
kuwachukulia hatua kali wabunge wa upinzani wanaosusia vikao vya Bunge,
Chadema, Kanda ya Magharibi, imemtaka Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
kujitafakari upya kama anafaa kuendelea na nafasi hiyo.
Kwa
nyakati tofauti, viongozi wa CCM na Chadema walitoa kauli hizo ikiwa ni
siku ya 12 tangu wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendesha na Dk
Tulia.
CCM
walisema kitendo kinachofanywa na Chadema kinachochea siasa za kibaguzi
badala ya kufanya kazi ya kutunga sheria ya kusimamia Serikali kwa
maslahi ya wananchi.
Katibu
wa Siasa Itikadi na uenezi Mkoa wa Mbeya, Bashuru Madodi aliwaambia
waandishi wa habari ofisini kwake kuwa kitendo kinachofanywa ni kinyume
cha maadili na mwongozo wa nchi na kumpongeza Dk Tulia kwa msimamo wake
wa kuliongoza Bunge bila kujali ubabaishaji wa wabunge wa upinzani.
“Kitendo
cha wabunge kutoka nje wakati wa vikao na kupiga soga ni utovu wa
nidhamu na kutoheshimu kiti cha spika na hivyo wajiulize bungeni
walikwenda kwa maslahi ya wananchi au la? ”alihoji.
Madodi
alisema pia halmashauri kuu inalaani vikali matamko yanayotolewa ya
wabunge wa upinzani ya kuzunguka nchi nzima kufanya siasa za kuwahadaa
wananchi kuwa wameonewa bila kutambua kuwa wao ni chanzo cha uvunjifu wa
amani kwa kutozingatia na kufuata kanuni na taratibu za Bunge.
Kadhalika alisema ni vyema Bunge kufanya maamuzi ya kutowalipa posho wabunge watakaokuwa wakishindwa kuhudhuria vikao vyake.
“Uongozi
wa Bunge usitetereke kwa vitendo vya ubabaishaji wa vyama vya upinzani
na uendelee kuchukua hatua stahiki dhidi ya wabunge wanaoendelea na
vitendo vya utovu wa nidhamu badala ya kuwasilisha kero za wananchi
waliowachagua,” alisema.
Kaimu
Katibu CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo alipongeza jitihada zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ya
kurejesha nidhamu ya utendaji wa kazi serikalini hali itakayosaidia
uchumi wa nchi kusonga mbele na kurejesha nidhamu.
“Haya
yote ni matunda ya Rais wa awamu ya tano kwa kweli anastahili pongezi
kwa uwajibikaji na utendaji wa kazi kwa watendaji ndani ya chama na
serikalini,” alisema.
Katibu
wa Chadema Kanda ya Magharibi, General Kaduma alimlaumu Tulia akidai
hana uchungu na wananchi kwa kuwa hakuchaguliwa kwa kupigiwa kura kama
walivyokuwa manaibu waliomtangulia.
Kaduma
alidai Naibu spika huyo amevunja kanuni za Bunge na kuwadhalilisha
wabunge wa upinzani kwa kushiriki kuondoa vipengele muhimu katika hotuba
ya waziri kivuli wa mambo ya ndani, Godbles Lema.
Katibu
huyo ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa Katibu wa Chadema Kanda hiyo,
Christopher Nyamwanji, aliitaka Serikali kuingilia kati uamuzi
uliotolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge akidai hayakuwa sahihi.
“Mchango
wa wabunge waliozuiliwa kuingia bungeni ni mkubwa katika Bunge hili la
bajeti ila utakosekana kutokana na uamuzi uliochukuliwa na naibu spika
ambao kimsingi unaminya demokrasia nchini,” alidai.
Pia,
alikemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na kutumia silaha
za moto kutawanya umma akisema kinasababisha uvunjifu wa amani.
Amelitaka
jeshi hilo kuacha kufanya kazi kwa maslahi ya CCM na badala yake wawe
walinzi wa amani nchini kwa kufanya kazi bila upendeleo.
Mwenyekiti
wa Chadema mkoa wa Tabora, Francis Msuka alisema wajibu wa kufanya
mikutano ya siasa nchini ni wa muda wote kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu
mwaka jana.
Alisema
kumekuwa na matukio ya viongozi wa Chadema kunyanyaswa na Jeshi la
Polisi huku viongozi wake ngazi ya vijiji wakifanyiwa mizengwe ili
wasitimize majukumu yao kikamilifu.
0 comments:
Post a Comment