Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara imetupilia mbali shauri la kupinga matumizi ya kanuni za maudhui ya kimtandao.
Kesi hiyo namba 25 ya mwaka 2018 ilifunguliwa na Baraza la Babari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Muungano wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu wote kwa pamoja wanapinga kanuni za maudhui ya kimtandao.
Katika kesi hiyo washtakiwa ni Waziri wa Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 9, 2019 na Jaji Wilfread Ndyansobera.
Katika maamuzi yake Jaji Ndyansobera amesema kwamba maombi ya wapeleka maombi hayana uzito.
Akizungumza baada ya maamuzi hayo, Wakili wa Mahakama Kuu upande wa wapeleka maombi, James Marenga amesema wanaheshimu uamuzi wa mahakama kwa niaba ya wateja wake lakini wataangalia nini cha kufanya.
“Tutazungumza na wateja wetu tuone ni namna gani nyingine tunaweza kufanya kama tutakata rufaa basi tutakwenda kwenye mahakama ya juu lakini tunaheshimu mahakama kwa sababu ndio taratibu za kisheria,” amesema Marenga
Kwa kawaida kanuni hizo zilipaswa kuanza kutumika rasmi Mei 5, 2018 lakini Mei 4, 2018 mwaka huu, Mahakama hiyo iliweka zuio la muda baada ya kuwasilishwa kwa shauri la kupinga.
Na Haika Kimaro, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment