Kikosi cha Biashara United
Tukiachana na namna Simba wanavyoendelea kunoga katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Azam FC kuchukua Kombe la Mapinduzi kwa mara ya tatu mfululizo, mitanange ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara inaendelea kila siku.
Kumekuwa na maendeleo makubwa kwa timu za Aliance FC na Biashara United tangu zilipofanya maamuzi mazito ya kutimua makocha wake mwishoni mwa mwaka uliopita kutokana na hali mbaya katika matokeo ya michezo yao.
Biashara United ilimtimua kocha wake Thiery Hitimana, Desemba 27 baada ya kuiongoza timu hiyo takribani mechi 16 na kuambulia mechi 11 pekee zilizoifanya timu hiyo kuburuza mkia katika msimamo wa ligi.
Lakini baada ya kuajiri kocha mpya Amri Said ambaye aliondoka Mbao FC, timu hiyo imefanikiwa kushinda michezo miwili na kwenda sare mechi moja, michezo ambayo imeifanya klabu hiyo kuondoka mkiani mwa ligi hadi katika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 17.
Alliance FC ambayo imesifika kwa kusheheni vijana, ilianza vema katika mechi za awali za ligi kabla ya kupotea kabisa katikati ya mzunguko wa kwanza, hali iliyopelekea timu hiyo kuwa katika nafasi tatu za mwisho za msimamo wa ligi.
Baada ya kumtimua kocha wake na kumsajili kocha mpya, Malale Hamsini, Alliance FC ikaanza kubadilika na kuwa klabu shindani katika ligi. Katika michezo mitano ya mwisho, Alliance imefanikiwa kushinda michezo mitatu na kutoka sare mechi mbili na kusogea hadi nafasi ya 12 ya msimamo wa ligi.
Hali hii inaonesha kuwa timu hizi zimebadilika kwa kiasi kikubwa na kuleta matumaini mapya kuwa huenda zikamaliza katika nafasi nzuri zaidi za ligi.
0 comments:
Post a Comment