MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei hizi zitaanza kutumika kuanzia leo Mei 4, 2022. Pamoja na kutambua bei hizo, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:-
(a) Bei za rejareja za petroli ni Shilingi 3,148 kwa lita kwa Dar es Salaam, Shilingi 3,161 kwa lita kwa Tanga na Shilingi 3,177 kwa lita kwa Mtwara;
(b) Bei za rejareja za dizeli ni Shilingi 3,258 kwa lita kwa Dar es Salaam, Shilingi 3,264 kwa lita kwa Tanga na Shilingi 3,309 kwa lita kwa Mtwara;
(c) Bei za rejareja za mafuta ya taa ni Shilingi 3,112 kwa lita kwa Dar es Salaam na bei za bidhaa hiyo kwa mikoa yote nchini zimekokotolewa kulingana na gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka miji husika.
(d) Mabadiliko ya bei yanatokana na ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia zinazochangia takribani asilimia 93 ya ongezeko la bei hizo na gharama za uagizaji (premium) ambazo zinachangia takribani asilimia 4. Vilevile, bei za mafuta hapa nchini zina uwiano na bei za bidhaa hizo katika nchi jirani.
(e) EWURA inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
(f) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi
stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
(g) Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (Price cap) au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama ilivyokokotolewa kwa kutumia fomula na Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia Magazeti ya Serikali Na. 2A na 57 ya tarehe 3 Januari 2022 na 28 Januari 2022, sawia.
(h) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.
Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.
(i) Wauzaji wa mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na Wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya aidha kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, na pia, risiti hizo zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya mafuta ya petroli.
0 comments:
Post a Comment