Monday, 16 May 2022

SPIKA WA BUNGE AWAKINGIA KIFUA WABUNGE 19 WALIOFUKUZWA CHADEMA..ASEMA 'JAMBO LAO LIPO MAHAKAMANI'

...

Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Tulia Ackson
Wabunge 19 wa CHADEMA waliovuliwa Uanachama
**

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson amewakingia kifua wabunge 19 wa kuteuliwa kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambao walivuliwa uanachama na Chama hicho Mei 12,2022 Jijini Dar es Salaam.


Akiongea Bungeni katika Bunge la 12 la Bajeti, Mkutano wa 7 kikao cha 23 amebainisha kama Spika amepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika ikimtaarifu juu ya maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho kuhusu kuwavua uanachama Wabunge 19 kutoka chama hicho.


Spika Tulia amesema Bunge haliwezi kuingilia jambo ambalo lipo Mahakamani na kwa mujibu wa Katiba ya nchi Mamlaka yenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki ni Mahakama, hivyo maamuzi ya Mahakama ndiyo yatakayotoa hatima ya Wabunge hao.


Spika Tulia amesisitiza kuwa maswali yeyote kuhusu jambo hilo mtu rasmi wa kuyajibia hayo ndani ya Bunge ni Spika wa Bunge na si mtu mwingine yeyote.


Hata hivyo baadhi ya wabunge kati ya 19 wa Viti Maalum waliofukuzwa uanachama na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameingia bungeni kuendelea kushiriki vikao vya Bunge.

Aliyeingia wa kwanza kuingia bungeni leo Jumatatu Mei 16, 2022 ni Sophia Mwakagenda ambaye aliingia kwa kutumia mlango wa kawaida akiwa ameongozana na wabunge wengine wa CCM na moja kwa moja kaingia ukumbini.

Mwakagenda kaingia viwanja vya Bunge saa 2.44 asubuhi akitumia geti la kawaida ambalo hutumiwa na wabunge wote.

Dakika sita baadae waliingia Grace Tendega na Conchesta Rwamlaza ambao wao walitumia mlango wa geti linalotumiwa na watumishi wengine maarufu geti la Waziri Mkuu.


Wabunge hao waliingia moja kwa moja hadi ndani ya ukumbi na kuketi katika viti vyao.

Muda mfupi baada ya kuanza shughuli za bunge, waliingia Taunza Malapo na Cecilia Pareso na kama ilivyo kwa wenzao walikaa kwenye Viti vyao na kila mmoja alifungua kishikwambi chake kufuatilia shughuli za bunge ambazo hutumiwa kidigitali kwenye vishikwambi.


Kwenye kipindi cha maswali Grace Tendega alipewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kuhusu ukubwa wa Jimbo la Kilolo akihoji ni lini Jimbo hilo ligawanywa kiutawala kwani ni kubwa.


Swali hilo limejibiwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi David Silinde akiomba wahusika wafuate taratibu zinazotakiwa na Serikali itakapojiridhisha italigawa Jimbo hilo.


Wengine walioingia bunge likiendelea ni Jeska Kishoa, Nusrat Hanje na Ester Matiko.


Ndani ya Bunge Jeska Kishoa alionekana akipita kwenye viti walivyokaa wenzake na kuwaonyesha simu yake kama kitu kilichokuwa kimeandikwa ili wasome.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger