Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Shaka Hamdu Shaka akielekeza jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Janeth Mayanja alipokuwa akizungumza na Wananchi baada ya kupokea changamoto mbalimbali za Wanancnhi wa Kata ya Gitting,Hanang waliofika kumsikiliza
**
Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Manyara
WANANCHI wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara wamesema wanampongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika kuleta maendeleo na kwamba wilaya hiyo wamepokea Sh.bilioni 20 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ndani ya mwaka mmoja tu.
Akitoa salamu kwa niaba ya wananchi hao, mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka ambaye ni mlezi wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja amesema wilaya hiyo kupitia Rais Samia na Serikali anayoingoza wamepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na utekelezaji mikubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Hanang tunakuomba Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi utufkishie salamu zetu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, huku kwetu tumepokea fedha nyingi za maendeleo.Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia tumepokea Sh.bilioni 20 za kutekeleza miradi, huko nyuma hatukuwahi kupatiwa fedha nyingi kwa kiasi hiki , tunashukuru na wananchi wa Hanang tunampenda sana , tunamuunga mkono,”amesema Mayanja.
Kuhusu changamoto, Mkuu huyo wa Wilaya amemueleza Shaka kwamba, moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo katika wilaya hiyo ilikuwa ni maji lakini tayari Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwenye maeneo ambayo yamekuwa na changamoto hiyo akitolea mfano kata ya Gitin.
“Katika kata ya Gitin kuna changamoto ya maji lakini tunakumbuka wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2020, Mama Samia alifika kwenye Wilaya yetu na alikuja Kata ya Gitin alituahidi kuwa changamoto ya maji itapata ufumbuzi.
“Leo sote tunashuhudia mradi wa maji ukiendelea kutekelezwa na tayari tumeshaanza kupokea fedha Sh.bilioni 2.2 kati ya Sh.bilioni tatu ambazo zinahitajika.Tunaamini ndani ya miezi sita mradi utakuwa umekamilika na wananchi kwenye maeneo ambayo mradi huu umepita hawatakuwa na shida ya maji.Yoye hata yanafanyika chini ya Rais Samia,”amesema Mayanja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang Mathew Dareda amesema wananchi wa wilaya hiyo wameendelea kufurahishwa na namna ambavyo Rais Samia amekuwa akiwatumikia katika kuleta maendeleo na imani yao kuna siku atafanya ziara kwenye Wilaya hiyo na kwamba Rais Samia anaupiga mwingi kutokana na maendeleo aliyowapelekea.
Baada ya salamu hizo za viongozi wa Wilaya hiyo, Shaka alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Hanang katika maeneo tofauti ambako alikwenda kukagua utekelezaji wa miradi likiwemo eneo la Gitin amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia imedhamiria kutatua changamoto za wananchi na kuboresha maisha yao.
“Kikubwa ndugu zangu wana Hanang, Manyara na Watanzania kwa ujumla tuendelee kumuunga mkono Rais Samia ambaye ana dhamira ya dhati kabisa ya kulitumikia taifa letu, amekuwa akifanya mambo makubwa ya kute maendeleo kila kona, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake amefanya makubwa yanayostahili kupongezwa.Niwahakikishie Rais Samia atatuvusha.
“Wakati nakuja huku nimewasiliana na Rais kwa njia simu, ameniambia maneno mawili tu kwanz anawapenda sana wananchi na pili anasema kazi iendelee na kubwa zaidi nchi yetu iko salama, imetulia.Niwaombe wananchi watoe ushirikiano kwa Serikali,”amesema Shaka.
Mbali ya kuzungumza na wananchi amepata nafasi ya kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo ambapo amepongeza kazi nzuri inayofanywa na viongozi ngazi ya wilaya kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe Janeth Mayanja akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto zilizotolewa na Wananchi mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Shaka Hamdu Shaka ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Manyara
Baadhi ya Wananchi waliofika kumsikiliza Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Shaka Hamdu Shaka ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Manyara.
0 comments:
Post a Comment