Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 20,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 20,2022
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imebaini dosari katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya wasichana Butengwa, ujenzi wa barabara za changarawe zilizo chini ya TARURA katika Manispaa ya Shinyanga na ujenzi wa shule mpya ya Usule na ujenzi wa Kituo cha Afya Salawe katika halmashauri ya Shinyanga.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kazi zilizofanywa na TAKUKURU katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Januari – Machi 2022) leo Ijumaa Mei 20,2022 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa amesema miradi hiyo ni sehemu ya miradi 18 ambayo TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha shilingi 13,794,801,486/= zilizotolewa na Serikali.
“TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za serikali katika miradi ya maendeleo 18 mkoani Shinyanga yenye thamani ya shilingi 13,794,801,486/= iliyoletewa fedha za Serikali ambayo ni miradi sita ya sekta ya afya, mitano sekta ya miundombinu, miwili elimu na mitano sekta ya maji. Kati ya hiyo 18 minne ilikuwa na dosari na 14 haikuwa na dosari”,amesema Mussa.
“Kati ya miradi mine iliyokuwa na dosari miradi mitatu dosari zake zilikuwa ndogo kiasi kwamba TAKUKURU ilitoa ushauri wa namna ya kuzifanyia marekebisho dosari husika kwa mamlaka husika”,ameeleza.
Ameitaja miradi iliyobainika kuwa na dosari ndogo ndogo ni mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Wasichana Butengwa Manispaa ya Shinyanga, ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Usule halmashauri ya Shinyanga, ujenzi wa Kituo cha Afya Salawe katika halmashauri ya Shinyanga na ujenzi wa barabara za changarawe zilizo chini TARURA Manispaa ya Shinyanga.
“Baadhi ya dosari zilizobainika kwenye mradi wa barabara baadhi ya maeneo katika barabara ya Bugweto – Ipeja kutokuchongwa na kushindiliwa vizuri,baadhi ya maeneo ya pembeni katika barabara ya Butengwa – Ning’wa kuharibika mapema kutokana na kutokushindiliwa vizuri na kutengenezwa wakati wa mvua”,amefafanua.
“Kwenye mradi wa shule mpya ya Sekondari ya Wasichana Butengwa tulibaini msingi ulichimbwa kwenda chini urefu wa sentimita 70 badala ya sentimeta 90 kama BOQ inavyoonesha na kwenye mradi wa shule mpya ya Sekondari ya Usule tulibaini kutokuwekwa njia za kupita watu wenye ulemavu kwenye baadhi ya majengo. Kwa upande wa ujenzi wa Kituo cha afya Salawe tulibaini dosari katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambapo uchunguzi umeanzishwa”,ameongeza Mkuu huyo wa TAKUKURU.
Amesema miradi 18 iliyokaguliwa bado utekelezaji wake unaendelea na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mmoja umeanzishiwa uchunguzi na kwamba wametoa elimu ya utekelezaji bora wa miradi hasa inayotumia Force Account kwenye maeneo ya uandikaji wa kumbukumbu za manunuzi,utunzaji nyaraka za miradi na utunzaji vifaa vya ujenzi.
Katika hatua nyingine amesema Dawati la uchunguzi la TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga limepokea taarifa 48 za malalamiko ambapo zinazohusu Rushwa ni 35 na tayari 17 uchunguzi wake unaendelea, 13 umekamilika na 5 uchunguzi wake umefungwa kwa kukosa ushahidi.
“Kesi zinazoendelea mahakamani ni 18 kati ya hizo kesi mpya ni tatu na katika kipindi cha mwezi Januari – Machi kesi 6 ziliamuliwa mahakamani na kesi 4 zilishinda kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kulipa faini”,amesema Mussa.
Mussa amesema kwa kipindi cha Mwezi Aprili hadi Juni 2022 TAKUKURU mkoa wa Shinyanga imepanga kukamilisha majukumu yake kwa kufanya uchunguzi na kujielekeza zaidi kwenye ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha iliyoletwa.
Ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuhakikisha miradi yote inayoendelea ikamilike kwa ubora na kama wataona vitendo vyovyote vinavyoashiria mashaka/ ubadhilifu wa miradi hiyo watoe taarifa kwa kufika Ofisi za TAKUKURU zilizopo Shinyanga au wapige simu namba 0738150196 au 0738150197 , Ofisi ya TAKUKURU Kahama 0738150198 na Ofisi ya Kishapu 0738150199
0 comments:
Post a Comment