Tuesday, 10 May 2022

MELI KUBWA ILIYOBEBA MAGARI 4397 YAWASILI BANDARI YA DAR ES SALAAM, YAVUNJA REKODI

...

Muonekano wa mbele wa Meli ya Meridian ACE ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam leo mchana.
Meli kubwa ya shehena ya magari inayojulikana kama Meridian ACE ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Nicodemas Mushi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, mara baada ya kuwasili kwa meli hiyo.
Meli kubwa ya shehena ya magari inayojulikana kama Meridian ACE ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam.
Muonekano wa nyuma wa Meli ya Meridian ACE ilipokuwa ikiwasili katika Bandari ya Dar es Salaam leo mchana.

MELI kubwa ya shehena ya magari yapatayo 4397 imewasili katika Bandari ya Dar es Salaam. Meli hiyo ya MERIDIAN ACEyenye idadi kubwa ya magari imewasili leo majira ya saa sita mchana na kuvunja rekodi, ikiwa na idadi kubwa ya magari kuwasili kwa mara moja katika Bandari hiyo. 

Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Eric Hamis, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Bw. Nicodemas Mushi alisema wanayofuraha kubwa kuipokea meli ya Meridian ACE, iliyovunja rekodi ya nyumba iliyowekwa mwezi mmoja uliopita ya kuwasili magari 4o41  mwezi Aprili 8, 2022.

Akifafanua zaidi, Bw. Mushi alisema meli hiyo imetokea nchini Japan na kupitia nchini Singapore na kuja moja kwa moja katika Bandari ya Dar es Salaam. "Kama ambavyo tumeshuhudia meli hiyo imetuletea magari 4397, huku asilimia 23 yaani magari 991 yatabaki nchini Tanzania na asilimia 77 yatakwenda nje ya nchi. 

Aliongeza kuwa magari yaliyosalia yanatarajiwa kupelekwa katika nchi za Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi pamoja na DR Congo.

"Niseme kwamba hii ni hatua muhimu inayoonesha imani ya Watanzania, wateja na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi, ambao kutokana na ubora wa kazi inayofanyika na imani ya wateja wetu kwenye eneo la ulinzi na usalama, ubora wa huduma pamoja na umakini unaofanyika katika utoaji wa huduma hizi. 

Aidha alisema kuwasili kwa meli hiyo kuna maana kubwa katika uchumi wa Tanzania, kwani ujio wa meli kubwa kama Meridian Ace ni ishara ya ufanisi mkubwa wa Bandari ya Dar es Salaam. Alibainisha kuwa ili kuweza kupata makampuni makubwa na mawakala wakubwa wenye mzigo kama huo ni lazima pawepo na imani ya watumiaji wa Bandari.

Alisema ujio wa meli hiyo ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za uboreshaji shughuli za bandari na uwekezaji mkubwa wa vifaa ambayo vimewekwa ili kuboresha huduma na ufanisi wa kazi bandarini. 

"...Mfano ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa vya kazi, vyote hivi vinaifanya bandari yetu sasa kutoa huduma katika kiwango cha juu kabisa cha ubora, itakumbukwa kwamba katika eneo la ulinzi na usalama tunafanya vizuri sana. 

"Mizigo ya wateja wetu yote inafika katika ubora na inaondoka bandarini kwetu ikiwa salama kabisa, habari hizi njema zinawafanya wateja wapya pamoja na wasiku zote kuendelea kuiamini bandari yetu...ikumbukwe kwamba menejimenti ya TPA ikiongozwa na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na ushauri na ulezi makini kutoka Wizara yetu Mama Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi...," alisisitiza.

"...Tunafanya kampeni kubwa za kimasoko ndani ya nchi pamoja na nje ya mipaka ya Tanzania lengo likiwa ni kutumia fursa zote zinazotuzunguka kuanzia nchi zote majirani zetu zinapitisha mzigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania." Alisema Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Bw. Mushi mara baada ya kuwasili kwa meli hiyo.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger