Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya chato wakiwa kwenye kikao cha Baraza.
Na Daniel Limbe, Chato
BARAZA la madiwani wa halmashauri ya Chato mkoani Geita, limedai kushtushwa na wizi wa fedha za serikali kwenye soko kuu la Buseresere kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali kudaiwa kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Baraza hilo kutaka kujua kiwango cha makusanyo ya fedha toka kwenye chanzo hicho cha mapato ya ndani, ambapo mwenyekiti wa kamati ya Uchumi,mipango na fedha, ambaye ni diwani viti maalumu Muganza,Retisia Isaya, alidai hana majibu ya swali hilo.
Awali Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Christian Manunga, alidai malengo ya ukusanyaji mapato ya ndani umefikia aslimia 71 kwa robo ya tatu ya mwaka hali inayotishia kutofikiwa malengo iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Akichangia hoja hiyo, Diwani wa kata ya Buseresere, Godfrey Miti, ameonekana kushangazwa na ripoti ya halmashauri hiyo kuonyesha kuwa soko la Buseresere halijukusanya hata senti moja kwa robo ya tatu ya mwaka,wakati shughuli za kibiashara zikiendelea kufanyika eneo hilo.
Amependekeza kamati ya Uchumi fedha na mipango kufanya uchunguzi sababu za kukosekana mapato ya serikali kwenye soko hilo ili watakaothibitika kutafuna fedha hizo wachukuliwe hatua za kisheria.
Hata hivyo, Diwani kata ya Kachwamba, Stella Kiwanuka,amekemea tabia ya kupotea kwa mapato ya halmashauri hiyo kutokana na baadhi ya watumishi wa Umma kutaka kujinufaisha pasipo kutazama maslahi mapana ya halmashauri hiyo.
"Mwenyekiti huu mchezo tunapaswa kuutafutia mwarobaini wa kudumu...haiwezekani soko la buseresere lisikusanye mapato hata senti wakati ndiyo chanzo kikubwa cha fedha kwa halmashauri yetu ikiwa ni pamoja na soko la Muganza na Chato"alisema
Ofisa habari halmashauri hiyo, Richard Bagolele, kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji, amedai taarifa hiyo imeandaliwa kutokana na kile kilichoonekana kwenye mfumo wa kupokea fedha za halmashauri hiyo.
0 comments:
Post a Comment