Saturday, 5 November 2016

Magufuli: Vyombo Vya Habari Simamieni Kujenga Maadili Na Utamaduni Wa Mtanzania

...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya Habari nchini kuwa mbele katika kusimamia Maadili na kuutangaza Utamaduni wa Mtanzania.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahojiano ya mwaka na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu aingie madaraka.

“Jukumu la kulinda Utamaduni na Maadili ya mtanzania ni la kila mzalendo, mtanzania, mzazi na Wizara husika ipo kwa ajili ya kusimamia jambo hili na vyombo vya habari mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kulisimamia kwa kuanzia katika vyombo vyenu vya Habari kutokana na kile mnachoonyesha”Alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alivitaka vyombo vya Habari kuwa wazalendo katika kutengeneza vipindi vyenye mahadhi ya kitanzania ili kuisaidia jamii kukua katika utamaduni wetu na kusaidia kujenga maadili yaliyo bora.

Mbali na hayo Rais Magufuli alizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi chake cha mwaka mmoja toka aingie madarakani ikiwemo kuongezeka kwa mapato kutoka bilioni 800 mpaka makusanyo ya shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi.

Pia alisema kuwa Bajeti ya mwaka 2016 ya trilioni 29.5 iliyotenga asilimia 40 kwenye miradi ya maendeleo imekuwa yenye mageuzi makubwa ukilinganisha na bajeti ya miradi hapo nyuma mabayo ilikuwa asilimia 26 tu.
Pamoja na hayo Rais magufuli alisema kuwa Serikali imeagiza ndege nyingine mbili zambazo inategemewa kufika nchini mwanzoni mwa mwaka 2018 ili kuboresha sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia uundwaji wa serikali alisema mategemeo yake katika serikali aliyoiunda imefanikiwa kwa kuwa Baraza aliloliunda la watu wachache limekuwa la mafanikio makubwa na hili limetokana na ushirikiano mkubwa wa mawaziri wake.

Rais Magufuli alivitaka vyombo vya habari nchini kubadili mtazamo wao katika uandishi wao wa habari na kuandika habari ambazo zina maslahi kwa Taifa na kuwahakikishia waandishi wa habari kushirikiana nao kwa kuwa anatambua kazi nzuri wanayoifanya.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger