Sunday 21 July 2019

Nec Kuanza Uboreshaji Wa Daftari La Kudumu La Wapiga Kura Julai 31, Mkoani Simiyu

...
Na Stella Kalinga, Simiyu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuanza rasmi zoezi la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Simiyu kuanzia  Julai 31, 2019 hadi Agosti 06, 2019.

Akifungua mkutano wa wadau wa Uchaguzi mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage amesema  Tume imekamilisha maandalizi ya uboreshaji daftari ambayo ni pamoja na kuhakiki vituo vya kujiandikisha, uandikishaji wa majaribio, maandalizi ya vifaa vya uboreshaji daftari, mkakati wa elimu kwa mpiga kura na uzinduzi wa uboreshaji wa daftari la kudumu  la wapiga kura.

Amesema  uboreshaji huu hautawahusisha wapiga kura wote walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015 bali utawahusu wapiga kura wapya ambao wametimiza miaka 18, wale ambao watatimmiza.umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi Mkuu mwaka 2020, ambao wamehama katika maeneo ya awali ya uchaguzi na wale ambao kadi zao zimeharibika

Katika hatua nyingine Jaji Kaijage ametoa rai kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi ili kuboresha taarifa zao, huku akitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa,  kuzingatia sheria za uchaguzi na kanuni zake katika zoezi hili la uboreshaji na maelekezo kwa Vyama vya Siasa kuhusu uboreshaji.

Kwa upande wake Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Frank Mhando amesema Tume imefanya uhakiki wa vituo vya uandikishaji ambavyo vimeongezeka kutoka 36,549 mwaka 2015 hadi 37,407 mwaka 2018 (Tanzania Bara), upande wa Tanzania Zanzibar vimeongezeka kutoka 380 mwaka 2015 hadi 407 mwaka 2018; huku akifafanua kuwa katika uandishaji huu kila Kijiji au Mtaa utakuwa na angalau Kituo kimoja cha kujiandikisha.

Naye Mratibu wa Zoezi la Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Mkoani Simiyu, Bw. Maganga Simon amesema mkoa umejiandaa vizuri ili kufanikisha zoezi ambapo wananchi wenye sifa zaidi ya 700,000 wanatarajia kuandikishwa katika daftari hilo huku akiwasisitiza viongozi wote mkoani hapo  kuwahamasisha wananchi wenye sifa kujitokeza kujiandikisha.

“Mkoa wetu ni mwenyeji wa Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka2019, tutatumia fursa hiyo kuhamasisha, kutakuwa na bango kubwa litakaloonesha kuwa kuanza  Julai 31 hadi Agosti 6 2019 mkoa wetu utashiriki kikamilifu kwenye  zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na Simiyu tumejipanga kufanikisha zoezi hili ambalo linasimamiwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi” alisema

Akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu,  Katibu wa Chama cha Viziwi (CHAVITA) Mkoa wa Simiyu, Alex Benson amewaomba viongozi wa vyama vya siasa kuwapa fursa watu wenye ulemavu kuwania nafasi mbalimbali, huku akisisitiza wasimamizi kupewa mafunzo ya lugha ya  alama ili kurahisisha mawasiliano  na watu wenye ulemavu pindi wanapoenda kujiandikisha na kupiga kura.

Naye Dora Stephano kutoka katika ASASI za kiraia amesema Tume ione uwezekano wa kuongeza ushirikishwaji wa asasi za kiraia nyingi zaidi, ili kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa wapiga kura juu ya masuala mbalimbali ya uandikishaji na uchaguzi.

Mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Simiyu, umewahusisha  Mratibu wa Uandikishaji wa Mkoa, Viongozi wa Vyama vya siasa Viongozi wa dini, wawakilishi wa watu wenye ulemavu, wawakilishi wa vijana, wawakilishi wa wanawake, wawakilishi wa asasi za kiraia, watendaji wa Tume na waandishi wa habari.
MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger