Saturday, 27 July 2019

Waziri Lugola Ataka Viongozi Wa Taasisi Zake Kuacha Kuwanyanyasa Askari, Watumishi Raia

...
Na Felix Mwagara, MOHA-Ifakara.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara yake nchini, kuacha tabia ya kuwanyanyasa askari waliochini yao na wahakikishe wanawapandisha vyeo, wanarekebisha mishahara, pamoja na kulipwa fedha za likizo.

Lugola amesema kuna idadi kubwa ya askari wanaostahili kupandishwa vyeo na kurekibishiwa mishahara, kwa kuwa Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli askari hao wana haki kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Askari na Watumishi wa Wizara yake, mjini Ifakara, Wilaya Kilombero, Mkoani Morogoro, leo, Lugola alisema katika uongozi wake hataki kusikia askari wananyanyaswa na kiongozi yeyote wa Taasisi zake.

Lugola alisema, unyanyasaji, kutokupandisha vyeo, pamoja na kulipwa fedha zao za likizo, changamoto hizo zinapunguza nguvu ya utendaji kazi wa askari hao wanaofanya kazi ngumu.

Waziri Lugola aliongeza kuwa, alitoa agizo la askari wanaostahili kupandishwa cheo, kurekebishiwa mishahara yao, wanaodai kulipwa fedha za uhamisho pamoja na changamoto mbalimbali zingine alizozielekeza.

 “Kwanini bado hamjapanda vyeo na kubadilishiwa mishahara yenu mpaka sasa wakati nilishatoa maelekezo mpandishwe, nitahakikisha nalifuatilia hili mapema zaidi ili nijue tatizo ni nini, lakini naamini kila kitu kinaenda vizuri na ahadi niliyoitoa itakamilisha kwa wale askari ambao wanasifa watapewa vyeo hivi karibuni,” Alisema Lugola.

Pia Lugola alizungumzia kuhusu ukosefu wa nyumba za makazi ya askari, kuwa licha ya Rais Dkt. John Magufuli anatoa mchango mkubwa kwa kulisaidia Jeshi, lakini bado kuna upungufu mkubwa wa nyumba hizo.

“Pamoja na fedha kidogo tunazopata lakini bado tuna tatizo la ukosefu wa makazi wa nyumba za askari, lakini bado Serikali inatafuta fedha ili kuhakikisha changamoto hiyo inaisha,” alisema Lugola.

Pia Lugola alisema changamoto nyingine inayowakabili askari wa vyombo vyake ni kutopata fedha za kuhamishwa na atahakikisha madai yote ya askari hao yanafanyiwa kazi.

Lugola alisema jambo ambalo linamuumiza kichwa ni kuhusu madai ya askari na watumishi wa wizara yake ambayo anasema kama wafanyakazi hawatalipwa haki zao na utendaji wa kazi utapungua.

Waziri Lugola yupo Mkoani Morogoro kikazi na tayari amemaliza ziara yake Wilaya ya Kilombero, na anatarajia kufanya ziara hiyo katika Wilaya za Malinyi na Ulanga Mkoani humo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger