Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Mbozi Mhr John Palingo kumkamata mfanyabiashara aliyewauzia wakulima mbegu feki katika wilaya hiyo hivyo kuathiri mavuno kwa wakulima.
Waziri Hasunga ameyasema hayo wakati wa mikutano yake katika kijiji cha Isalalo, Wasa na Malolo vilivyopo katika kata ya Wasa kadhalika akiwa katika kijiji cha Msia, Weru 1 na Iganduka vilivyopo katika kata ya Msia.
Waziri huyo wa Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa kitendo cha mtu kuuza pembejeo feki ni cha uhujumu wa Kilimo na uchumi na kwamba serikali haiwezi kuvumilia hali hiyo.
"Katika hili namwagiza mkuu wa wilaya kumkamata msambazaji wa mbegu hizo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa" alisema Hasunga.
Kauli hiyo ameitoa kufuatia swali la mkulima mmoja mkazi wa Kijiji cha Malolo Ndg Isaya Nyondo ambaye alitaka kujua hatua zipi zinachukuliwa na serikali kufuatia kuuziwa mbegu feki na hivyo kufanya washindwe kuvuna mwaka huu.
Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kuimarisha sekta ya Kilimo hivyo mfanyabiashara yeyote anayecheza na ufanisi wa wakulima atachukuliwa hatua Kali za kisheria.
0 comments:
Post a Comment