Na. Mwandishi Wetu.
Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imetoa ufafanuzi kuhusu Mwandishi wa kujitegemea Erick Kabendera baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kuwa amekamatwa na anahojiwa kuhusu uraia wake na Idara ya Uhamiaji Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Idara ya Uhamiaji Gerald Kihinga, amesema kuwa Erick Kabendera ameshikiliwa na Jeshi la Polisi na Uhamiaji Jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi ili kuweza kupata taarifa juu ya uraia wake.
Kamishna huyo wa Uhamiaji amesema Idara ya Uhamiaji inadhamana kubwa ya kusimamia na kutekeleza Sheria ya uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002, inayotoa mamlaka kwa taasisi hiyo kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote.
“Idara ya Uhamiaji ni chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutekeleza na kusimamia uraia wa Tanzania, kwa hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo, sisi tunamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake, na siyo yeye tu aliyefanyiwa hivyo, idara ya Uhamiaji inatimiza matakwa ya sheria ya uraia nchini na wala si vinginevyo” Alisema.
Alieleza kuwa idara ya Uhamiaji ilipata taarifa za Erick Kabendera kutoka kwa raia wema na ikaamua kumtafuta ili kufanya naye maojiano lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kukataa kufika ofisi za Uhamiaji, hali iliyopelekea kukamatwa na sasa anaendelea kuhojiwa.
Mkuu huyo wa masuala ya uraia na Pasipoti alifafanua kuwa, kushikiliwa huko kwa Erick Kabendera na kuendelea na mahojiano ni swala ambalo limekuwepo kwa raia wote ambao uraia wao una utata, wakiwemo watu wa kawaida, watu mashuhuri na wengine wowote ambao kutaonekana uhitaji.
Amesema kumekuwa na ushirikiano baina ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikwemo Polisi, ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiusalama kwa nchi hivyo kukamatwa kwa Kabendera siyo jambo geni bali Idara inatimiza majukumu yake chini ya Sheria ya uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002.
0 comments:
Post a Comment