Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango Benny Mwaipaja, ameeleza kutokea kwa kifo cha mfanyakazi mwenzao, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Mhandisi Leopold Lwajabe, ambaye mwili wake umekutwa ukiwa umening'ínia juu ya mwembe Wilayani Mkuranga.
Mwaipaja akitoa taarifa hiyo amesema, mtumishi huyo kwa mara ya kwanza alitoweka Julai 16 na kupatikana, na baadaye alitakiwa kwenda kuripoti kituo cha polisi Mburahati kwa lengo la kueleza ni kipi kilimsibu.
''Ni kweli tukio limetokea alikuwa ni mtumishi wa Idara ya Fedha za Nje, Julai 25 aliaga ofisini kwamba anaenda polisi Mburahati na toka hapo hakuonekana tena, ndio leo tumepata taarifa tumefika eneo la tukio tumekuta mwili wake umening'ínia juu ya mwembe, sasa mwili wake unapelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi kisha masuala mengine ya mazishi yafuate'' amesema Mwaipaja.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Mkoa wa kipolisi Rufiji RPC Onesmo Liyanga, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, lakini bado wanaendelea kufuatilia ili kujua alikuwa na nafasi gani wizarani.
''Hatujapata data vizuri kama alikuwa na nafasi gani katika utumishi wake, kwa sababu hata kuutambua huo mwili imechukua muda, kwahiyo bado na ndugu ndio walikuwa wanakuja, kwahiyo naomba tupeane muda kwa kusaidiana na ndugu zake tutatoa taarifa na taarifa zote zitapatikana'' amesema RPC Liyanga.
0 comments:
Post a Comment