Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog Bukoba
Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini mkoani Kagera,Mhe. Wilfred Muganyizi Rwakatare (CHADEMA) amekanusha uvumi wa kwamba amejiunga na Chama cha Wananchi CUF.
Akitolea ufafanuzi huo leo Julai 30,2019 Rwakatare amesema hivi karibuni kumekuwepo na uvumi ambao umekuwa ukiendelea katika mitandao ya kijamii uliomtaja kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Mbunge huyo amesema kuwa siasa kama siasa ina maneno mengi yakiwemo yenye uzushi pale mwanasiasa amekuwa anapoungana na wenzake wa vyama tofauti hasa katika masuala ya kimaendeleo.
Amesema kuwa hivi karibuni alikwenda kwenye ofisi za CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es salaam kwa lengo la kuwasalimia baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo mwenyekiti wa chama hicho Prof. Ibrahimu Haruna Lipumba ndipo uvumi kuwa kajiunga na CUF ulipoanza kusambaa mtandaoni.
Rwakatare ameongeza kuwa aliwahi kuwa kiongozi wa chama cha CUF kama Naibu katibu mkuu wa chama na wakati anaondoka kwenda CHADEMA,na aliondoka pasipo kuwa na chuki na mtu yoyote ndani ya chama na ndiyo maana wakati anakwenda kuwasalimia alipokelewa kwa furaha na shangwe.
Amewataka watu wanaozusha uvumi huo kuacha tabia hiyo mara moja na kuwataka kumfuata mlengwa ili aweze kutolea ufafanuzi wa jambo husika na kuacha tabia za kuvujisha taarifa za kupotosha umma wa Watanzania huku akiongeza kuwa hata siku za nyuma aliwahi kuzushiwa kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM.
Katika hatua nyingine,Rwakatare amewataka wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini kuunga mkono jitihada za maendeleo katika kipindi hiki ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa likiwemo suala la miundombinu za barabara, afya, shule, ukarabati wa meli mpya, michezo , pamoja na ujenzi wa stendi kuu mpya ya mabasi ambayo inajengwa katika kata ya Kyakailabwa mkoani Kagera.
0 comments:
Post a Comment