Monday, 29 July 2019

THRDC Yawataka Watu Ambao Sauti Zao Zimedukuliwa na Kusambazwa Mitandaoni Wafungue Kesi Mahakamani

...
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umewataka watu ambao sauti zao zimedukuliwa na kusambazwa mitandaoni kufungua kesi mahakamani.

Umesema kesi hizo zikifunguliwa, wahusika wanaweza kuwashtaki watu au taasisi wanazodhani kuhusika kwa maelezo kuwa kitendo hicho ni kinyume na katiba ya Tanzania.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushauri wa hali ya faragha na usalama wa mawasiliano.

"Suala la mawasiliano binafsi limelindwa kikatiba na kisheria kama haki ya faragha, zipo mamlaka ambazo zimeruhusiwa na sheria kuweza kuchukua taarifa binafsi za mtu kwa matumizi maalamu  lakini hazipaswi kubadilika kuwa za umma," alisema Olengurumwa.

Kauli hiyo ya THRDC imekuja zikiwa siku chache baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saeed Kubenea, kutaka TCRA kuwachukulia hatua wanaohusika na vitendo hivyo vya udukuzi.

Kubenea alisema hayo baada ya kudaiwa kuwa mawasiliano Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba, yamedukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Jambo hilo lilibuka baada ya Kinana na Makamba kumwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, wakilalamikia kile walichodai kuwa wamedhalilishwa na mwanaharakati Cyprian Musiba.

Olengurumwa alisema serikali inapaswa kutunga sheria hiyo ili kuepusha ukiukwaji wa haki ya faragha itakayoendana na Katiba ya Tanzania na mikataba mingine ya kimataifa kuhusu haki ya faragha na mawasiliano.

Alisema kifungu cha 16 (1) cha Katiba ya Tanzania kinaeleza kuwa: "Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi."

Pia alisema THRDC inawataka watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha wanalinda heshima ya biashara zao kwa kulinda taarifa za faragha za wateja wao na kwamba wananchi ambao haki zao za faragha zimevunjwa wanapaswa kwenda kufungua kesi mahakamani.

"Watu wote ambao haki yao ya faragha imevunjwa, wanahimizwa kufungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda yoyote nchini, kuwashtaki watoa huduma au watu binafsi walioingilia kwa namna yoyote kudukua na kutumia mawasiliano hayo bila hati ya ruhusa ya mahakama," alisema Olengurumwa.

Alisema watu hao wanaweza kwenda kufungua kesi na kushtaki watoa huduma za mawasiliano kwa kuwa ni kosa kuvujisha mawasiliano ya mtu bila ya lidhaa.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger