Friday 19 July 2019

Katibu Mkuu Ofisi Ya Waziri Mkuu Akutana Na Wakuu Wa Taasisi Kujadili Namna Bora Ya Utekelezaji Wa Mpango Kazi Wa Mwaka 2019 - 2020

...
NA; MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe amekutana na Wakurugenzi wa Taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo kwa lengo la kujadili kwa kina maeneo watakayo shirikiana kwa pamoja katika mpango kazi wa mwaka 2019 – 2020 na kutoa maelekezo juu ya namna bora ya kuhudumia wananchi kulingana na huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano uliopo jengo la PSSSF Jijini Dodoma, alisema kuwa Mwaka wa fedha 2019/2020 ni muhimu kukubaliana kwa pamoja maeneo ambayo yatatekelezwa kwa ushirikiano ili kuimarisha utendaji wa shughuli mbalimbali.

“Lengo kuu la kukutana kwetu hapa ni kuangalia utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kwenye mpango kazi wa kila Taasisi katika mwaka huu wa fedha, na kubaini namna bora ya kutekeleza maeneo hayo kwa ufanisi,” alisema Massawe.

Katibu Mkuu aliongeza kuwa kupanga na kukubaliana maeneo ya ushirikiano katika utekelezaji wa mpango kazi kutasaidia kuongeza tija katika utendaji wa kazi na majukumu ya kila siku.

 “Ninapenda kuona tunakuwa mfano wa kuingwa kwa kujijengea mwenendo mzuri wa kushirikiana katika utendaji ili kufanikisha shughuli nyingi kwa wakati mmoja,” alisisitiza Massawe

Aidha, alitoa wito kwa wakuu hao kuzingatia suala la mawasiliano na uhusianao kwa wadau na wateja wanaowahudumia ikiwemo kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa kwa wakati.

Kwa Upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama Mahala Pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda alieleza kuwa ushirikiano na taasisi nyingine na wizara ni fursa pekee itakayo wawezesha kutekeleza dhamira na mikakati waliyopanga ili kuleta maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba alisema kuwa yapo maeneo mengi ya kushirikiana kwa pamoja na mpango kazi wa mwaka ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio yatakayo wasaidia kuwa na ushirikiano endelevu katika maeneo mbalimbali.

Kikao hicho kiliudhuriwa na Wakurugenzi na Wataalamu wa Mipango na Bajeti kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger