Friday 19 July 2019

Aweso Anusa Harufu Ya Rushwa Na Upigaji Dili Mradi Wa Maji Masange Kondoa Uliogharimu Zaidi Ya Tsh.mil.433

...
Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Naibu Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso amesema  Wizara yake itashirikiana na TAKUKURU  ili kujiridhisha  katika  utekelezaji mradi wa Maji kijiji cha Masange Wilayani Kondoa mkoani Dodoma Uliogharimu zaidi ya  Sh.Milioni 433  baada ya kupewa majibu yasiyojitosheleza na Mkandarasi wa Mradi huo.
 
Naibu Waziri Aweso ameyasema hayo   Julai 18,2019 katika kijiji cha  Masange Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo alipofanya ziara ya kukagua na kujionea mradi wa Maji kijiji cha  Masange uliogharimu kiasi cha Sh.Milioni  mia nne  thelathini na tatu,laki mbili,themanini na nane elfu,mia tano ,arobaini nane[433,288,548].
 
“Haiwezekani  tukauziwa mbuzi kwenye gunia,lazima kukagua na kujionea,baada ya kupewa majibu ya kusuasua hivyo TAKUKURU tutashirikiana nao  kubaini ubadhilifu,na mkandarasi asilipwe mpaka tufanye uchunguzi tujiridhishe”alisema Aweso.
 
Hali hiyo imekuja baada ya Mkandarasi wa mradi huo wa Maji kampuni ya Best One kwa kushirikiana na wataalam wa sekta ya Maji wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kutoa majibu yasiyoridhisha kuhusu matumizi ya fedha zilizotumika katika mradi huo .
 
 Mhe.Aweso amepiga simu mbele ya wananchi kuulizia taratibu za upatikanaji wa Gari la kuchimba visima .
 
Mbunge wa Kondoa ambaye  pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  Dokta.Ashatu Kijaji amesema yupo tayari kufanya  kazi hata saa sita usiku na walichomwagiza wananchi wake ni kutatua kero ya Maji .
 
Wananchi wa Mtaa wa Masange wamesema adha kubwa inayowakabili ni maji hivyo ni  vyema serikali ikafanya mchakato haraka  kutatua kero hiyo.
 
Awali ,akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Masange mbele ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso,Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji vijijini[RUWASA]Wilaya ya Kondoa Mhandisi Falaura Seleman Kikusa  amesema mradi wa Maji Masange ulianza tangu tarehe 15,Disemba,2014 na kuzinduliwa rasmi tarehe  13,Septemba ,2016 kupitia  mbio za Mwenge wa  Uhuru huku ukigharimu zaidi ya Tsh.Milioni 433 .
 
Aidha amebainisha kuwa muda wa utekelezaji wa Mradi huo kwa mujibu  wa Mkataba  ni kipindi cha miezi mine  kuanzia tarehe 15,Disemba,2014,hadi 15,Machi,2015 hivyo kutokana na changamoto mbalimbali hususan kuchelewa kwa malipo ya madai ya mkandarasi,mradi uliongezewa muda wa utekelezaji   na kukamilika rasmi mnamo tarehe 7,Juni,2018.

Mhandisi  Kikusa ameendelea kufafanua kuwa upatikanaji wa Maji katika kijiji cha Masange haukidhi mahitaji halisi ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho kwani huduma ya maji imekuwa ikipatikana kwa mgao  kwa vitongoji kwa masaa manne hadi matano.
 
Amesema chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo unatokana na changamoto kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa wakazi  pamoja na kukua kwa mji  wa Masange ,Uwezo wa chanzo cha Maji [lita   119,577.6 kwa siku]kuwa mdogo ikilinganisha na mahitaji halisi ya Maji ya sasa [zaidi ya lita 141,560  kwa siku]  na changamoto  nyingine ni usimamizi usio mzuri kutoka kwa timu ya mhandisi .
 
Hata hivyo mkandarasi   wa mradi hadi kufikia sasa alishalipwa kiasi cha sh.347,421,000  kati ya gharama 433,288,548 na zilizobaki kwa mujibu ya makubaliano ya mkataba ni Tsh.120,609,648.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger