Friday, 18 January 2019

Wizara ya Madini Kuweka Msukumo Miradi Ya Liganga, Mchuchuma

...
Na Asteria Muhozya, Ludewa
Wizara ya Madini imesema itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kuweka msukumo ili kuhakikisha  kwamba miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Linganga inaanza kutekelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa Januari 16 na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za madini mkoani Njombe  na kuona namna ya kutatua changamoto zinazohusu Wizara ya Madini katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema miradi hiyo ni moja ya miradi ya kimkakati ambayo Taifa linatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa, hivyo kutokana na umuhimu wake, wizara ya madini itashirikiana na wizara hiyo kuhakikisha hatua zaidi zinapigwa ili hatimaye miradi hiyo ianze kutekelezwa kwa kuwa imechukua muda mrefu.

Aliongeza kuwa, ni miradi mikubwa ambayo taifa linatarajiwa kunufaika nayo  kupitia ajira na kuongeza pato la nchi huku akiyataja madini ya chuma kuwa moja ya malighafi muhimu kwa uchumi  wa Tanzania ya viwanda na kusema kuwa, kama taifa, linautolea macho mradi huo na kwamba serikali imedhamiria kuutekeleza.

Aliongeza kwamba, katika Serikali ya Awamu ya Tano, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anayo imani kubwa  kuwa miradi hiyo itaanza huku serikali ikitegemea kupeleka maendeleo kwa wananchi kupitia miradi husika.

“Wizara yetu ndiyo inatoa leseni za madini na tayari tulishatoa leseni ya Makaa ya mawe mchuchuma kwa hiyo nimefika kuangalia changamoto ambazo ziko upande wa wizara yetu kuweza kuzitatua ili tutoke hapa. Miradi hii tumeisikia miaka mingi ni wakati sasa tunataka ianze.” alisisitiza Nyongo.

Aliongeza kuwa, ikiwa wizara ndiyo inatoa leseni za madini,  inaowajibu wa kujua yule aliyepewa leseni kama anaifanyia kazi na kuongeza, “Sisi tuliotoa leseni lazima tuangalie tuliyempa leseni amekwama wapi  lakini pia tujue miradi hii inaanza lini? Makaa ya mawe na chuma vyote vinahitajika kwa taifa. Tunatambua makaa ya mawe ni madini ambayo yana tija kwa uchumi kwa nchi,” alisema Nyongo.

Akifafanua zaidi kuhusu miradi hiyo alisema kuwa, mradi wa Makaa ya Mawe unatarajiwa kuzalisha umeme ambao mbali ya kuuza kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umeme huo unatarajia kutumika katika kuzalisha madini ya Chuma Liganga.

“ Mpango ni Liganga kutumia megawati 250 kwa shughuli zake za kuzalisha chuma na megawati 350 zitauzwa Tanesco kuzalisha umeme,” aliongeza.

Akifafanua sababu za kuchelewa kwa miradi hiyo, alisema ni kutokana na changamoto za kimkataba ambazo bado ziko katika majadiliano katika ngazi za juu na kuitaja baadhi ya mikataba hiyo kuwa ni  kuwa ni pamoja na mikataba ya upunguzaji wa kodi.

Aliongeza kuwa, wizara ya madini ikiwa ni wizara ambayo inasimamia Sheria ya Madini, imelenga kuhakikisha kwamba miradi hiyo mikubwa inaanza ili hatimaye iweze kuwanufaisha watanzania na taifa.

Akielezea suala la fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo, alianza kwa kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kwa kutenganisha suala la miradi hiyo na fidia  ambapo alisema kwamba taratibu za juu zikikamilika, wananchi watalipwa fidia na hivyo kuwataka kuwa na subira na kuwa tayari kupisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali,  Mkuu wa Mkoa wa Njombe , Christopher Ole Sendeka alimweleza waziri umuhimu wa wizara ya madini kujielekeza  kwenye kupata taarifa halisi kuhusu tafiti zilizofanyika awali kuhusu akiba iliyopo ya madini ya chuma Liganga na Makaa ya Mawe mchuchuma.

Aidha, aliongeza kuwa, mbali na chuma na makaa ya mawe mkoa huo unayo madini mbalimbali ikiwemo dhahabu ambayo bado haijachimbwa kwa kiasi kikubwa.

Miradi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga, inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda Group Ltd, ya China.

Pia, akiwa mkoani humo, Naibu Waziri alitembelea mgodi wa Kokoko Kokoto wa Nyakamtwe Quary, ambapo alitoa changamoto kwa mmiliki wa mgodi huo kuongeza kasi ya uzalishaji na kuwa wabunifu kutumia fursa  za miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa na serikali ikiwemo ya ujenzi wa reli ili kokoto hizo ziweze kutumika.


from MPEKUZI http://bit.ly/2VZbx4W
via Malunde
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger