Bodi ya Tumbaku nchini imeagizwa kuhakikisha kuwa Wakulima wote wa zao hilo wanasajiliwa katika mfumo unaoeleweka kwani hilo ni lengo la haraka la Wizara kwa taasisi zote la kuwasajili wakulima wote nchini ili kujua kiasi cha maeneo wanayolima.
Hayo yameelezwa jana tarehe 17 Januari 2019 na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa wadau wa sekta ndogo ya Tumbaku katika ukumbi wa Mwanakiyungi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mhe Hasunga ameitaka Bodi ihakikishe kwamba tumbaku yote itakayovunwa msimu huu inauzwa ifikapo Juni 2019 sambamba na kuagiza masoko kuwahi kuanza msimu huu ili kurahisisha kuanza mapema maandalizi ya zao hilo msimu wa 2019/2020.
Vilevile Waziri Hasunga ameagiza upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. “Hili linaenda sambamba na utekelezaji wa Agizo la Mhe: Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) – Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuhakikisha unakuwepo utaratibu wa kumwezesha mkulima anajitegemea kwa pembejeo ili aache kuwa tegemezi wa mikopo ya mabenki” Alikaririwa Mhe Hasunga
Mhe Hasunga alisisitiza kuwa lazima Bodi kutilia mkazo malengo ya muda mrefu kwenye Tumbaku ambayo ni pamoja na utafutaji wa masoko (mhakikishe mnapata wanunuzi wengine wapya ifikapo 2022), Kuhakikisha kuwa kwa ubia au ushirikiano uliopo kijengwe kiwanda kipya cha kuchakata tumbaku ili kutoa ushindani wa gharama za uchakataji wa tumbaku nchini, Kuongeza ubora wa zao kutoka asilimia 87 ya sasa hadi asilimia 92 ifikapo June 2022 na Kuongeza mbegu mpya na bora za tumbaku ili kuweza kupenyeza katika masoko ya nchi zingine kama China n.k.
Tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu matano ya kimkakati ya biashara katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe: Dkt. John Joseph Pombe Magufuli – Rais waJamhuri ya Muunganowa Tanzania. Mazao hayo ni Tumbaku, Kahawa, Pamba, Korosho, na Chai. Takwimu zinaonesha kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 hadi kufikia mwaka 2016 tumbaku imekuwa na mchango mkubwa kuliko mazao mengine makuu ya biashara kwa kuliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
“Natambua juhudi mnazofanya katika hifadhi ya mazingira. Lakini mnatakiwa muongeze juhudi kwani taarifa zinaonesha kuwa hadi kufikia msimu wa kilimo uliopita wa 2017/2018 wastani wa miti iliyopona baada ya kupandwa na wakulima ni asilimia 40.46 tu, kiwango hiki hakiridhishi maana kiko chini mno” Alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema Ili uzalishaji wa tumbaku uwe katika mtazamo wa kibiasharawataalam mnapaswa kuwaelimisha wakulima ili waelewe kwa dhati umuhimu wa kuzingatia taratibu za kilimo cha tumbaku (Compliance).
Alisema kuwa Baadhi ya wakulima katika vyama vya msingi vya ushirika wameshindwa kulipwa malipo yao kutokana na vyama kuwa na madeni yasiyokuwa wazi na yasiyolipika. Hali hii imesababishwa na ubadhirifu wa baadhi viongozi na watendaji wasio waaminifu katika ushirika, utoroshaji na ulanguzi wa tumbaku.
Moja ya maeneo yanayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na masuala yanayohusu hatua za kutatua changamoto za kulikomboa zao la tumbaku na kulipa sifa zinazohitajika katika soko la dunia. Mfano wa masuala hayo ni pamoja na Wingi na ubora wa zao, Kuongeza tija, Malipo stahili kwa wakulima, Utunzaji wa Mazingira na Kuzuia utumikishwaji wa watoto.
Kupitia mkutano huo Waziri wa Kilimo amebainisha kuwa Serikali iko thabiti kusimamia uendelevu na uzalishaji wenye tija wa zao la tumbaku kama zao mojawapo la biashara la kimkakati. Ni kwa msingi huo, Serikali inaendelea na jitihada za kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili tasnia ya tumbaku.
“Tarehe 28-30/12/2018 niliwaita viongozi wa Bodi za mazao ikiwa ni pamoja na Bodi ya Tumbaku na kuwapa malengo ya muda mfupi (Januari – Juni, 2019) na mrefu (Julai – Juni, 2022) ni pamoja na nyie wadau katika nafasi zenu mshirikiane ili kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa” Alisisitiza
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe Agrey Mwanri alisema kuwa mkutano huo maalumu wa mwaka wa wadau wa Tumbaku ni mkutano ambao upo kwa mujibu wa sharia ya sekta ya Tumbaku Na 24/2001 kifungu cha 49 cha marekebisho ya sheria yam waka 2009 ambao imeweka ulazima wa wadau kukutana walau mara moja kwa mwaka kujadili masuala mbalimbali ya kuendeleza sekta hii na kutatua changamoto zilizopo na kukubaliana utaratibu wa ugharamiaji wa majukumu ya pamoja ambayo yameainishwa na sharia ya sekta ya Tumbaku.
Alisema uwepo wa mkutano huo umekuwa miongoni mwa mikutano yenye tija kwa kukutanisha madau wote na kuwa na mikakati ya pamoja, kuongeza ufanisi wa masoko ya Tumbaku, na uhai wa kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa pamoja.
Kwa upande wake Mzee Hassan Wakasuvi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa bodi ya Tumbaku akitoa taarifa ya utangulizi wakati wa mkutano huo alizitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Tumbaku kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa mkakati utakaotekeleza na shirikishi wa uhifadhi wa mazingira, kuchelewa kwa upatikanaji wa mikopo ya pembejeo kwa ajili ya kununua pemebejeo za kilimo.
Zingine ni utaratibu wa upatikanaji wa bei ya zao la Trumbaku katika kuhakikisha kuwa bei inapatikana mapema na kwa wakati, kushuka kwa mahitaji ya Tumbaku katika soko la Dunia, Kushuka kwa ubora wa Tumbaku ambao unachangiwa na masuala mbalimbali, Vita dhidi ya matumizi ya Tumbaku Duniani na kuboreka kwa bei ya pembejeo.
Sambamba na hayo pia ameishukuru serikali kwa mchango wake kwenye sekta ya Tumbaku kwa ushirikiano inaouonyesha katika suala la kuhakikisha kuwa wanapatikana wasambazaji wa pembejeo za kilimo na kufanikiwa kupunguza bei ya pembejeo za kilimo kwa msimu wa mwaka 2018/2019.
from MPEKUZI http://bit.ly/2Di68P5
via Malunde
0 comments:
Post a Comment