Mkuu wa Wilaya ya Masasi Selemani Mzee amelazimika kufanya kikao cha dharula na baadhi ya wakulima wa Vyama vya Msingi vya Ushirika AMCOS, baada ya baadhi ya wakulima kufika ofisini kwake wakilalamikia kuhusu ulipwaji wa fedha zao za korosho.
Kwa mujibu wa madai ya wakulima hao ni kwamba zoezi la uhakiki wa mashamba ambao lilitangazwa na serikali limekuwa likilegalega huku baadhi yao wakishindwa kulipwa fedha zao licha ya kuuza korosho yao kwa serikali.
Akizungumza kwenye mkutano huo na baadhi ya wakulima na viongozi wengine vyama hivyo vya msingi, Mkuu wa Wilaya amekiri kusuasua kwa zoezi hilo na kudai atalifanyia kazi.
"Nawaomba muwe wavumilivu kwa kuwa kila mkulima ambaye ni mkulima halali, lazima atalipwa fedha zake," amesema Mzee.
"Kuhusu suala la ukaguzi wa mashamba, hili nitakaa na wahusika kujua tatizo liko wapi, lakini ni lazima serikali iwalipe wakulima kupitia taratibu zake ambazo zinalenga kuhakikisha anayelipwa ni mkulima halali," ameongeza Mzee.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Wilaya, mmoja wa wakulima hao ambaye ameuza korosho zake kwenye Chama cha Msingi Tuaminiane (AMCOS), Saidi Khatau, alisema ni miongoni mwa wakulima wanaotakiwa kufanyiwa ukaguzi wa mashamba yao. Alisema wanashangaa kuona ahadi ya serikali ya kukagua mashamba yao haitekelezwi licha ya kuuza korosho.
0 comments:
Post a Comment