KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetangaza kuusimamisha Uchaguzi Mkuu wa Yanga uliopangwa kufanyika Jumapili hii kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo imefikia hatua hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa baadhi ya wanachama wa Yanga wamefungua kesi mahakamani wakitaka uchaguzi huo usimamishwe.
Akitangaza uamuzi huo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Malangwe Mchungahela, amesema: “Leo tulikuwa kwenye vikao vya mwisho kuangalia kama mambo yote yamekaa sawa.
“Tukiwa kwenye vikao hivyo, tukapata taarifa kwamba kuna baadhi ya wanachama wa Yanga wamefungua kesi ya kusimamisha uchaguzi hapa Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Morogoro na sehemu nyinginezo.
“Sasa sisi kama kamati hatutaki kugombana na muhimili wa mahakama na kwa sababu tumesikia sehemu zingine mashauri yameanza kusikilizwa, tumeamua kusimamisha uchaguzi usifanyike Jumapili hii mpaka tupate muongozo wa kilichojiri huko mahakamani.
“Jumatatu tutawapa msimamo wa uchaguzi, lakini kwa sasa kamati ya uchaguzi imesitisha uchaguzi huo kwa muda na wala hatujaufuta. Wale wagombea waliokuwa wakipiga kampeni tumewaambia wasimame kwanza.”
Uchaguzi huo wa Yanga ulikuwa na lengo la kujaza nafasi za uongozi klabuni hapo zilizoachwa wazi ambapo ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watatu.
0 comments:
Post a Comment