Tuesday 22 January 2019

TANESCO YAALIKA WAWEKEZAJI ZAIDI KWENYE VIWANDA ARUSHA

...

Meneja wa TANESCO jijini Arusha Mhandisi Herini Mhina(kushoto), akimsikiliza Meneja wa Shirika hilo wilaya ya Ki-TANESCO Mirerani, Mhandisi Zacharia Masatu, akifafanua kuhusu namna TANESCO ilivyoweza kufikisha umeme wa kutosha kwenye eneo la Mirarani Januari 21, 2019. 
***

UWEKEZAJI kwenye miundombinu ya umeme uliofanywa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO umeanza kuzaa matunda eneo la machimbo ya madini Mirerani mkoani Manyara.

Serikali kupitia TANESCO iliwekeza kwa kujenga kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha KIA na hivyo kuwezesha hali ya upatikanaji umeme ulio bora na wa uhakika kwenye eneo la Mirerani kuongezeka.

Kwa sasa matumizi ya umeme kwenye eneo lote la Mirerani ni kiasi cha Megawati 3.5 lakini kubwa zaidi miongoni mwa watumiaji wakubwa walioanza kufaidika na uwekezaji huo ni pamoja na kiwanda cha Godmwanga Gems Limited kinachojihusisha na kuchimba na kuchakata madini ya Kinywe (Graphite) na kile cha Mirerani Tanzanite vyote viko Mirerani.

Meneja wa Shirika la Umeme wilaya ya Ki-TANESCO Mirerani Mhandisi Zacharia Masatu amewaambia waandishi wa habari wanaotembelea eneo hilo kuwa kiwanda hicho pekee kinatumia kiasi cha Megawati 1.1 ya umeme.

Aidha Meneja wa TANESCO jijini Arusha Mhandisi Herini Mhina amesema jiji lina ziada ya umeme Megawati 50, na hivyo amewahimiza wawekezaji katika sekta ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo kuwekeza ili kufaidi uwekezaji wa serikali katika miundombinu ya umeme nchini.

“Wito wetu kwa wafanyabiashara na wawekezaji, waje wawekeze kwenye mkoa wetu wa Arusha sababu kama tulivyoeleza awali tuna umeme wa kutosha, kwa mkoa mahitaji ni Megawati 75 na uwezo wa kituo chetu ni Megawati 120 kwahiyo unaweza kuona tuna ziada inayofikia Megawati 50” ,lisema Mhandisi Mhina.

Mhandisi Mhina alibainisha kuwa, viwanda vinaweza kuleta matokeo makubwa ya uwekezaji katika miundombinu ya umeme uliofanywa na serikali kwani matumizi ya kiwanda kimoja inaweza kuwa ni mahitaji ya wilaya nzima.

“Viwanda ni njia mojawapo inayoweza kutupeleka kwenye uchumi wa kati tunaotaka kwa haraka zaidi”, alisisitiza.

TANESCO ilifunga mitambo ya kuingiza umeme wa kutosha kwenye kiwanda cha Godmwanga Gems Limited na kwamba kinajitegemea ambapo kuna jumla ya transfoma pozo kubwa tatu na gharama za ufungaji wa mitambo hiyo zinakadiriwa kufikia shilingi Milioni 60.

Aidha afisa wa kiwanda hicho cha kuchimba na kuchakata madini ya Kinywe (graphite), Nai Mainga alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa madini hayo ya graphite (kinywe) Juni 2018 na kwamba tangu uzalishaji uanze hadi hivi sasa, tayari wamezalisha kiasi cha tani 5,600 na wateja wakubwa wa madini hayo ni China.

“Matumizi makubwa ya madini hayo ya kinywe hutumika kutengeneza vitu maka betri na tunapozungumzia betri ni pamoja na betri zile kubwa za magario na mitambo, lakini pia kuna taarifa kuwa madini hayo hutumika kutengeneza bati maalum la kuzuia injini ya ndege ili isipate moto sana kwani madini haya huchomwa sana ili kupata zao la mwisho”, alifafanua.

Alisema kuna baadhi ya nchi ambazo tayari zimeanza mchakato wa kusitisha matumizi ya petrol kuendeshea magari na hivyo kuna uwezekano wa kutumia madini haya ili kutengeneza betri za kuendesha magari.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger