Monday, 7 January 2019

SPIKA NDUGAI AMTAKA CAG KUFIKA MBELE YA KAMATI YA MAADILI KWA HIARI LA SIVYO ATAPELEKWA KWA PINGU

...
Spika wa Bunge Job Ndugai amemtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad kufika mbele ya kamati ya maadili ya Bunge Januari 21, 2019 kwa hiyari vinginevyo atapelekwa kwa pingu.


Kwa upande wa Mbunge wa Kawe Halima Mdee ametakiwa kuripoti kamati hiyo Januari 22. Viongozi hao wa umma wanatuhumiwa na Spika Ndugai kulichafua bunge.


Miongoni mwa tuhuma hizo ni ile iliyotolewa hivi karibuni na Profesa Assad alipokuwa akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.


Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.


CAG alijibu: "Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.


"Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa."

Akiendelea kufafanua jibu lake, CAG Assad alisema: "Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua."

Mwaka 2018 lilipoibuka suala la upotevu wa Sh1.5 trilioni kwenye hesabu za Serikali mwaka wa fedha 2016-2017, Assad aliulizwa kuhusu nini kifanyike, akataka Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger