Thursday, 17 January 2019

SERIKALI YAANIKA MAENEO VIPAUMBELE KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

...
Na. WAMJW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imebainisha maeneo muhimu yaliyowekewa kipaumbele katika bajeti ili kuboresha miundombinu na hali ya upatikanaji wa Huduma za afya nchini.

Akieleza taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya wizara kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba, 2018 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma, Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Mh. Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge kupokea na kutumia bajeti ya jumla ya shilingi bilioni 866.24 ambapo Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 304.44 ilikua ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo shilingi 88.47 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 216.7 kwa ajili ya Mishahara ya watumishi walio makao makuu ya Wizara pamoja na Watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.


Waziri Ummy amesema fedha zilizopokelewa katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2018 zimeainishwa katika utekelezaji wa majukumu ya wizara katika kipindi hicho ambapo maeneo muhimu kama Chanjo, afya ya mzazi na mtoto, mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, upatikanaji wa damu salama, uimarishaji wa huduma za kibingwa, Utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali za Kanda, Maalum, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na uhakiki ubora wa huduma za afya yalipewa kipaumbele.


Aidha, Waziri Ummy amesema Wizara imeendelea kusimamia na kuratibu shughuli zilizokuwa zimepangwa kutekelezwa na Taasisi zilizopo chini yake. Taasisi hizo ni pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Mabaraza ya Kitaaluma.


Hata hivyo, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa Majukumu ya Wizara (Idara Kuu ya Afya), Waziri Ummy amebainisha changamoto mbalimbali zikiwemo Vituo vya kutolea huduma za Afya kutowasilisha mahitaji ya dawa, Vifaa, Vifaa tiba na Vitendanishi kwa wakati, Upatikanaji wa Huduma Bora na za Uhakika za Uzazi Mama na Mtoto, Upungufu wa watumishi wenye taaluma ya kutoa huduma za afya ikilinganishwa na mahitaji, Wigo mdogo wa wananchi walio katika mifumo ya Bima za Afya pamoja na Kuongezeka kwa watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger