Tuesday, 15 January 2019

RAIS MAGUFULI ASITISHA MARA MOJA ZOEZI LA KUONDOA VIJIJI NA VITONGOZI MAENEO YA HIFADHI

...
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Januari, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bi. Dorothy Mwanyika. 

Pamoja na agizo hilo Mhe. Rais Magufuli ametaka viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima ambao kwa sasa wanataabika kupata maeneo ya kufugia wanyama na kuzalisha mazao.

Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya zoezi la uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi, na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa.

“Mimi sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama kuna eneo ambalo tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki, tutabadilisha sheria, tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji, vivyo hivyo hata kwa wakulima kama kuna eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala wanyamapori, na lina rutuba, na wakulima wanataka kulima nalo tunalimega tunawapa wakulima.

Baadaye tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi, hili ni la mifugo, hili ni la wakulima, hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi Mawaziri na Makatibu Wakuu mkakae mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi nakadhalika, lakini pia tunahitaji wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za wanyama tunazimaliza, hapana, hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ameagiza vijiji vyote 366 vilivyoainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi hapa nchini visiondolewe katika maeneo hayo na badala yake ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amefafanua kuwa ni lazima Serikali ifanye maamuzi haya sasa kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka hadi kufikia Milioni 55, idadi ya mifugo imeongeza hadi kufikia Milioni 35 na hivyo kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi ikilinganishwa na wakati nchi inapata uhuru ambapo Watanzania walikuwa Milioni 9 na mifugo ilikuwa Milioni 10.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza sheria ya vyanzo vya maji pia iangaliwe upya ili kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando mwa mito na ameelezea kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya wakulima kwa madai kuwa wamelima ndani ya mita 60.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha kwake mapendekezo ya kufutwa kwa mashamba ambayo hayajaendelezwa na ameagiza wizara hiyo iendelee kumpelekea mapendekezo ya mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi wagawiwe kwa ajili ya kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amesema maagizo hayo hayana maana kuwa sasa wananchi waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka zoezi la uwekaji wa mipaka lifanyike haraka na kwa uwazi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
15 Januari, 2019
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger