Wednesday, 2 January 2019

RAIS MAGUFULI ASHIKA NAFASI YA PILI ORODHA YA VIONGOZI BORA AFRIKA

...
Rais John Magufuli ameshika nafasi ya pili kati ya marais watano bora Afrika kwa mwaka 2018 kutokana na kazi aliyoifanya ndani ya miaka mitatu ya utawala wake, jarida la mtandaoni la Africa54 limebainisha.

Jarida hilo lilifanya utafiti wake kwa kuuliza wasomaji wake nani ni Rais bora kwa mwaka wa 2018, kiongozi ambaye hafanani na viongozi wengine wa Afrika; ufanisi wake katika kazi, msimamo, ujasiri na uongozi na matokeo makubwa.

Africa54 limebainisha kwamba, Rais Magufuli amefanya maajabu katika muda wa miaka mitatu ambao amekaa madarakani kuliko kiongozi mwingine. Ameweza kutoa elimu bure, amefufua shirika la ndege na kununua ndege saba, ameanza kujenga reli ya kisasa (SGR) na ameongeza upatikanaji wa huduma za afya. Pia anafahamika kwa kupiga vita rushwa na ufisadi.

Nafasi ya kwanza kwa mujibu wa utafiti huo imechukuliwa na Rais wa Botswana, Ian Khama. Jarida hilo limeandika Rais Khama ni kiongozi mtulivu ambaye ameleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi ikiwamo kuboresha miundombinu, upatikanaji wa huduma za jamii na upatikanaji wa ajira nchini kwake.

Limesema licha ya kuwa kiongozi huyo amestaafu Aprili mwaka huu, bado Waafrika wengi wanamuona kama kiongozi bora ambaye hana mfano barani Afrika.

Nafasi ya tatu imekwenda kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ambaye aliingia madarakani Aprili mwaka huu inaonyesha kuwa alipendwa ghafla na wananchi wengi nchini humo.

Africa54 limesema kiongozi huyo amefanikiwa kuibadilisha Ethiopia kuwa nchi ya kidemokrasia zaidi na jamii iliyo huru.

Ghulib-Fakim wa Mauritius anachukua nafasi ya nne miongoni mwa marais bora wa Afrika. Jarida hilo linabainisha licha ya kuondolewa madarakani kwa kashfa ya kadi ya malipo, alisimamia haki na maendeleo ya watu katika nchi yake.

Nafasi ya tano inakwenda kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda. Limesema licha ya kiongozi huyo kuminya demokrasia, Waafrika wengi wanampenda kwa sababu amefanikiwa kulibadilisha Taifa lake kuwa kitovu cha uchumi Afrika Mashariki.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger