Picha ya Dk. Bayoum, mke wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, ambayo ameiweka mtandaoni akiwa kwenye hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha, imezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii watu wakimponda kwa kufanya hivyo.
Kigwangalla alituma picha hiyo ya mke wake kwenye ukurasa wake wa Instagram iliyokuwa na ujumbe unaosema kuwa Ngorongoro siku zote huwa hapachoshi kutembelewa na ndiyo sababu huwa yeye Waziri hakosi kutembelea mbuga hiyo kila mwaka.
Dk. Kigwangalla aliendelea kuandika kuwa maeneo hayo yanavutia na kumfanya mtu anayetembelea mbuga hiyo kuwa wa tofauti na kuwahimiza Watanzania wajenge utamaduni wa kwenda huko.
Picha hiyo ilimwonyesha kwa nyuma mke wake aliyekuwa amevaa fulana nyeusi na suruali yenye mabaka meusi na meupe akiangalia mandhari ya mbuga hiyo.
Wachangiaji kwenye ukurasa wake wa Instagram walianza kutiririka na hoja wakimponda kuwa alikuwa akitangaza maumbile ya mke wake badala ya kutangaza utalii ambao hauonekani kwenye picha aliyoituma.
Picha hiyo ilimwonyesha mke wake akiwa anaangalia madhari ya hifadhi ya Ngorongoro iliyokuwa ikionekana mawingu na sehemu kidogo ya maji na miti.
Clara Masanja ni mmoja wa watu waliomwomba Dk. Kigwangalla kufuta picha hiyo kwa sababu alizodai kuwa inamdhalilisha mke wake na wala haitangazi utalii.
“Kaka yangu Kigwangalla tunatoka wote Puge (Puge Madukani) mimi ni ukoo wa Wapandanzuki (Nzuki), Dk. Nzuki ni mtoto wa baba yangu mkubwa) babu mkubwa kwa babu mdogo). Nakushauri hii posti yako itoe haiko vizuri kabisa kaka yangu,” alisema Clara katika ukurasa huo wa facebook.
Pia alieleza kuwa Kigangwalla ni taswira kubwa katika jamii na watu wanategemea kujifunza mengi kutoka kwake, hivyo picha kama hizo zinaweza kumharibia sifa.
Mchangiaji mwingine, aliandika kuwa: “Mheshimiwa hapo hakuna anayesikiliza maneno yako ya utalii bali kila mtu yupo bize kuangalia maumbile ya mke wako. Wewe ni kioo cha jamii. Tunajifunza nini kutoka kwako kama kiongozi wa juu kabisa mwenye dhamana?” aliongeza.
“Hapo Mkuu unatangaza vitu zaidi ya viwili. Tafakari wakati mwingine watafute wenye kazi zao na si mke wako kwa upande mmoja,” alisema Donnell Pellagio.
Hata hivyo, Dk. Kigwangalla aliamua kufuta picha na maelezo aliyokuwa ameweka kwenye ukurasa wake huo wa Instagram na Facebook baada ya kuona imesambaa na kuzua mjadala.
0 comments:
Post a Comment