Wednesday, 23 January 2019

Picha : RAFIKI SDO YAKABIDHI VITENDEA KAZI VYA MILIONI 19.4 KWA WAWEZESHAJI WA VIKUNDI SHINYANGA

...
Shirika la RAFIKI SDO ‘Rafiki Social Development Organization’ limekabidhi vitendea kazi ikiwemo baiskeli 76 na mabegi 76 vyenye thamani ya shilingi milioni 19.4 kwa wasichana na wanawake ‘Wawezeshaji wa vikundi’ kwenye wilaya ya Shinyanga ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri katika mitaa na vijiji wanavyohudumia.

Hafla fupi ya makabidhiano ya vitendea kazi hivyo imefanyika leo Jumatano,Januari 23,2019 katika ofisi ya RAFIKI SDO mjini Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

Awali akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa RAFIKI SDO, Gelard Ng’ong’a alisema vitendea kazi hivyo vitatumika kwenye kata ambako shirika lao linatekeleza shughuli za miradi ya maendeleo na kuongeza kuwa baiskeli hizo zinakamilisha idadi ya baiskeli 148 kwani tayair walishatoa zingine 72.

“Wawezeshaji hawa 76 tuliwapa elimu,sasa wanakwenda kuunda vikundi vya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 kwa ajili ya kuwafundisha masuala ya ujasiriamali,malezi,mabadiliko ya tabia na masuala mtambuka,watatumia vitendea kazi hivi kuwafikia wananchi kwenye maeneo yao kwenye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga”,alisema Ng’ong’a.

“Shirika letu limeajiri wawezeshaji wa vikundi 131 kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2019,kati ya 72 ni wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na 59 halmashauri ya Shinyanga,tunawapatia mishahara kila mwezi,wanalipiwa NSSF na wameunganishwa na mfuko wa huduma za afya”,aliongeza Ng’ong’a.

Kwa upande wake,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko alilipongeza shirika la RAFIKI SDO kwa kushirikiana na serikali katika shughuli za maendeleo huku akibainisha kuwa shirika hilo linatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwezesha wananchi kiuchumi.

Mboneko aliwataka Wawezeshaji hao kutumia vyema vitendea kazi walivyopatiwa ,kuomba mikopo kwenye halmashauri na kuhakikisha wanatumia mikopo hiyo kwa shughuli za maendeleo.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo pia kuwahimiza wanawake kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto huku akiwashauri kutumia mikusanyiko ya watu kutangaza na kuuza bidhaa wanazotengeneza.

Aidha aliwaagiza maendeleo ya jamii kutembelea vikundi vilivyoanzishwa na kuvishauri huku akizitaka halmashauri kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyo mstari wa mbele kwenye masuala ya maendeleo.

Nao wawezeshaji hao walilishukuru shirika hilo kuwa karibu nao na kueleza kuwa hivi sasa wameweza kuanzisha biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kujiinua kiuchumi lakini pia tabia hatarishi zimepungua na wanaendelea kupaza sauti juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Muonekano wa baiskeli zilizotolewa na Shirika la RAFIKI SDO kwa Wawezeshaji wa vikundi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimkabidhi begi na baiskeli Anna Kulwa kutoka kijiji cha Kizungu kata ya Lyamidati halmashauri ya wilaya ya Shinyanga . Wa kwanza kushoto ni Afisa Maendeleo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Deus Mhoja na Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga, Jackson Njau, wa kwanza kulia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa RAFIKI SDO, Gelard Ng’ong’a wakishuhudia zoezi la makabidhiano ya vitendea kazi. 
Anna Kulwa akishikana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa RAFIKI SDO, Gelard Ng’ong’a.
Muonekano wa mabegi yakiwa kwenye baiskeli.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akikabidhi vitendea kazi kwa  Rahim Ibrahim kutoka kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.
Baiskeli na mabegi yaliyotolewa na RAFIKI SDO kwa wawezeshaji wa vikundi. 
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vitendea kazi vilivyotolewa na shirika la RAFIKI SDO kwa Wawezeshaji wa vikundi katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga. Kulia ni Afisa Tawala wilaya ya Shinyanga, Charles Maugira.
Mkurugenzi Mtendaji wa RAFIKI SDO, Gelard Ng’ong’a akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi kwa wawezeshaji wa vikundi.
Kulia ni Msaidizi wa Meneja shirika la RAFIKI SDO, Neema Lweeka akielezea kuhusu shirika hilo na shughuli za maendeleo wanazotekeleza hususani miradi ya afya,elimu,uwezeshaji kiuchumi,ulinzi wa mtoto,haki na utawala na utoaji elimu ya stadi za maisha.
Wawezeshaji wa vikundi wakifuatilia matukio yaliyokuwa yanaendelea.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akifurahia jambo na Wawezeshaji wa vikundi waliopatiwa vitendea kazi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiagana na wawezeshaji wa vikundi.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger