Upande wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Da es Salaam kuchoshwa na maelezo ya upande wa mashtaka kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Wakili wa utetezi, Hassan Kiangio, ameieleza mahakama hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Wanjah Hamza, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP kwa ajili ya kutolewa maamuzi.
Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh. milioni 785.6.
Washtakiwa hao wamekaa rumande kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.
Washtakiwa hao walifikishwa Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 17, 2016 kujibu mashtaka yanayowakabili.
“Kesi hii ni ya muda mrefu, wateja wangu wanaendelea kusota rumande bila kujua hatima yao, tumechoshwa na hizi kauli za upande wa mashtaka kuwa jalada lipo kwa DPP linafanyiwa kazi, tunataka wenzetu wa upande wa mashtaka watuambie wamefikia wapi juu ya upelelezi wa kesi hii,” Kiangio aliiambia mahakama hiyo.
Akitolea ufafanuzi wa hoja hizo, Wakili wa Serikali, Elia Athanas, alidai kuwa kesi hiyo iliitishwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada halisi la kesi hiyo lipo kwa DPP, hivyo wanasubiri uamuzi wake.
Novemba 15, mwaka jana, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, aliieleza mahakama kuwa wapo katika hatua za mwisho za uandaaji wa nyaraka ili kuipeleka kesi hiyo katika hatua nyingine.
Hakimu Mkazi, Hamza baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 15, 2019 itakapotajwa na kusema kuwa hoja za upande wa utetezi zitafanyiwa kazi na Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba, atakaporejea kutoka likizo.
0 comments:
Post a Comment