Mkazi wa kijiji cha Kateka, Kalambo mkoani Rukwa, Linus Mayaya (35) ametiwa matatani kwa kudaiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne kisha kumweka kinyumba.
Linus ameingia kwenye wakati mgumu kutokana na tuhuma hizo baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu mwanafunzi huyo huku akimpatia fedha za chipsi na soda ili kuweka mazingira ya kumsogeza karibu ili kutimiza azma yake.
Tukio hilo la kusikitisha na kushangaza jamii, limetokea baada ya mama mzazi wa mwanafunzi huyo, kutoa taarifa polisi kutokana na mtoto wake kuachishwa masomo na kijana huyo kumweka kinyumba akimfanya mke hali akifahamu kuwa anastahili kupata haki yake ya elimu.
Oliver Edita, mama mzazi wa mtoto huyo, alisema baada ya kutomwona mwanawe kwa siku mbili, alimtafuta huku na kule kisha juzi akabaini kuwa amewekwa kinyumba na mtuhumiwa huyo.
Alisema baada ya kugundua hilo, alitoa taarifa kwa serikali ngazi ya tarafa na polisi ambao walimkamata mtuhumiwa akiwa na mwanafunzi ndani mwake.
George Kyando, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema jeshi lake limemnasa mtuhumiwa huyo ambaye anaendelea kuhojiwa katika kituo kikuu cha polisi wilaya na atafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.
0 comments:
Post a Comment