Vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Kigoma vimemtia mbaroni kiongozi wa Shirika la Danish Refugees Services linalotoa usaidizi wa huduma za kibinadamu kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi za Nduta wilayani Kibondo na Mtendeli wilayani Kakonko.
Kiongozi huyo anatuhumiwa kuhusika na uingizwaji na uwagawaji wa nguo zinazofanana na sare za jeshi ndani ya kambi hizo za wakimbizi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga wakati wa uchomaji wa nguo uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kawawa mjini Kigoma, ambapo alisema kuwa kiongozi huyo anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa uchunguzi zaidi.
Bila kumtaja jina kiongozi huyo, Anga amesema kukamatwa kwake kunatokana na Mkuu wa Makazi katika kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilaya Kibondo kutilia shaka uwepo wa nguo hizo na mgawanyo wake.
Ndipo baada ya kufuatilia kwa kina akagundua kuwa nguo hizo zinafanana na sare za jeshi hivyo kuarifu kamati za ulinzi na usalama na nguo hizo kukamatwa kabla hazijaanza kugawanywa.
“Katika hatua ya awali tunamshikilia kiongozi wa Taasisi ya Danish Refugees Services ambaye kwa namna moja au nyingine anahusika na uingizwaji wa nguo 1,947 kwenye hizo kambi za wakimbizi na uchunguzi zaidi unaendelea, taarifa itatolewa baadaye kuhusiana na yale yanayoendelea kwenye suala hilo,” alisema.
Na Fadhili Abdallah - Habarileo Kigoma
0 comments:
Post a Comment