Sunday, 20 January 2019

Makonda Amwandikia WARAKA Mzito Tundu Lissu

...
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  ameandika waraka mzito akimponda Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,  ambaye kwa sasa yupo ziarani barani Ulaya baada ya kupata nafuu kufuatia shambulizi la kupigwa risasi alilofanyiwa Septemba 7, 2017 nyumbani kwake Dodoma.
 
Makonda ameandika; ACHA NISEME NAWE KIDOGO KAKA YANGU TUNDU LISSU HASA NIKIANZA NA Shukran kwake muumba wa mbingu na ardhi kwa kumpa kaka yetu Tundu Lissu afya na siha njema.
 
Wengi walioko jimboni Singida na wa Tanzania wote walihangaika kwa sala na maombi, usiku na mchana, Wengine wakichanga pesa zao na Hatimaye Mola akajibu maombi yao.
 
Kwa heshima na kuonyesha uzalendo, nakushauri Kaka yangu Tundu Lissu rudi nyumbani utoe shukrani zako kwao. Watu wako wamekumiss zaidi ya hao unaowakimbilia hivi sasa.
 
Ziara yako huko haina tija kwa yoyote, na kuichafua Serikali si kumchafua Mh. Rais ni kuichafua TANZANIA yetu sote na wewe ukiwemo. Jimboni kwako haujakuwepo muda mrefu, ni vizuri kwa kuwa Mungu kakujaalia afya basi ukaitumia kuwasikiliza na kuwasaidia watu wa jimboni kwako ambao ni Watanzania.
 
Huko uliko wanamatatizo yao na hawajawahi kuja TANZANIA kutueleza matatizo yao. Zaidi wanakuona kama kituko japokua hawawezi kukuambia.
 
Ikiwa ni lazima sana kuisema Tanzania dhidi ya kile unachokiita ubaya, na ni lazima useme kwa hao waliowatesa na kuwauwa Babu zetu basi Naomba usiache kuwaambia na haya; Shirika letu ya ATCL sasa limefufuka, sasa tuna ndege mpya sita (6), na ndege mbili (2) zikiwa njiani.
 
Ikiwa Lazima sana uwaambie pia ya kwamba ile mikataba mibovu iliyokuwa inapelekea shirika la Tanesco kufa na kufikia hata umeme kukatika katika, gharama kubwa na usiotabirika, sasa Rais Magufuli anajenga “Stiegler’s Gorge” yenye uwezo wa kuzalisha Megawatts zaidi 2,100 kwa wakati mmoja.
 
Ikiwa Lazima sana useme, basi waeleze kwamba mafisadi mwisho wao ulishafika, tulikuwa hatuna mahakama ya mafisadi, sasa tuna mahakama ya mafisadi na wahujumu uchumi. Mafisadi na wahujumu uchumi sasa wanafikishwa mahakamani.
 
Ikiwa ni lazima sana waeleze, naomba usisite pia kuwaambia Watoto wa masikini na wanyonge sasa wanasoma bure kuanzia darasa la kwanza mpaka Kidato cha nne.
 
Ndugu yangu na kaka yangu mpendwa Tundu Lissu, kama Lazima sana ukae na hao wazungu uwaeleze, Naomba uwaambie pia ya kwamba sasa miundo mbinu na barabara zinajengwa kila kona ya nchi ya Tanzania, hata utakaporudi Tanzania utapita kwa Flyover ya Mfugale.
 
Ikiwa ni Lazima sana waambie, basi usiache pia kuwaambia ya kwamba mashirika ya umma pamoja na mikataba iliyokuwa imeingiwa ya makampuni,  sasa hivi serikali inapata dividend.
 
Ikiwa ni Lazima sana waambie, wale Wanyama Tembo na Twiga waliokuwa wakisafirishwa na kuuwawa sasa hawasafirishwi tena kwenye ndege, wala hawauwawi na wapo salama hivyo waje kutembelea Tanzania tunahitaji watalii.
 
Ikiwa ni Lazima sana waambie basi Tanzanite inapatikana Tanzania tu, tena Arusha pale na duniani kote ni kwetu tu Tanzania. Tumejenga ukuta sasa kuhakikisha Tanzanite inalindwa na sasa thamani ya Tanzanite inaonekana kwenye mchango wa pato la Taifa.
 
Ndugu yangu na kaka yangu Mpendwa, Kama ni lazima sana waambie, yale madini waliyokuwa wanayasafirisha kwenye makontena na kutuambia ni mchanga tu, sasa yanabaki ndani ya nchi yetu na tayari taifa limeanza kunufaika. Na wale wajanja wanaosafirisha kwa kutorosha wanakamatwa, juzi tu hapa wamepelekwa mahakamani.
 
Ndugu yangu Tundu Lissu, Kama ni lazima saana waambie, waambie basi miradi ya maji kutoka ziwa Victoria, Miradi ya maji Dar es salaam, Miradi ya maji Mbeya, sasa hivi maji yanapatikana na kadri siku zinavyokwenda Raisi anazidi kutenga fedha kuhakikisha wananchi wanapata maji.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie basi migogoro ya wafugaji na wakulima imepungua sana na hawachinjani tena watanzania, wanakaa mezani wanayamaliza.
 
Lakini kama ni lazima sana uwaambie, waambie basi kwamba Raisi Magufuli anapanua tena bandari ya Dar es salaam kuhakikisha kwamba zile meli kubwa zenye mizigo mikubwa au mizigo mingi zinakuja kwenye bandari ya Dar es salaam.
 
Kama ni Lazima sana uwaambie, basi naomba uendelee kuwaambia ya kwamba Tanzania mpya inakuja, Tanzania mpya inajengwa, na Tanzania mpya ni ya watanzania wote.
 
Ndugu yangu Tundu Lissu, nakukaribisha tena, unaporejea tena katika taifa letu, taifa hili la Tanzania utakuta tayari terminal 3 Airport imeishaanza kufanya kazi na usisahau kupiga selfie maana nyumbani kumenoga.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie tangu mwaka 1909 ilipokuwa inajengwa reli ya kati kwa ajili ya kusafirisha mpira kutoka congo kuleta bandari ya Dar es salaam na wajerumani, sasa awamu hii raisi Magufuli anajenga reli ya Standard Gauge tena kwa fedha zetu za ndani.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie wafanyakazi sasa wanafurahia mifuko ya hifadhi na mafao yao. Misharaha ya wafanyakazi haicheleweshwi tena.
 
Kama ni Lazima sana uwaambie, waambie Viwanja vya ndege vinajengwa na Rada kulinda anga letu zinajengwa na usalama wa nchi unazidi kuhimarishwa
 
Usisahau tena kuwaambie bujeti ya Afya imeongezwa sana, Hospital na vituo vya afya vinajengwa, huduma za mama na mtoto pamoja na wazee zimeboreshwa, madawa yanapatikana sasa mahospitalini.
 
Wakati unakaribia kuwaaga na unataka kuwaambia la mwisho, basi waambie wamachinga wana vitambulisho vya kuwafanya wafanye kazi bila kubugudhiwa wala kusumbuliwa na yeyote. Waambie pia wamachinga wana pia bima za afya.
 
Ndugu yangu Tundu Lissu, kama ni lazima sana ukae na hao wazungu uwaeleze, waeleze basi habari za bomba la mafuta linajengwa kutoka Uganda kuelekea Kwetu Tanga kuimarisha uchumi wetu kwa ujumla.
 
Kama ni Lazima sana uwaambie, waambie serikali ya Tanzania ni ya Viwanda, viwanda vinajengwa na watanzania wana pata Ajira .
 
Kama ni lazima sana uwaambie, basi waambie kwamba sasa hivi Tanzania mfumuko wa bei umeshuka ( inflation).
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie basi ndugu yangu, usisite basi na unapokuwa unataka kusema hayo unayotaka kuyasema naomba na mimi nikuongezee mengine ya kwangu na ya watanzania tulioko huku tunaojua kinachoendelea. Kama lazima sana useme waambie Interest rate imeshushwa na watanzania wanaendelea kukopa.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie hakuna njaa tena Tanzania, chakula kipo cha kutosha mpaka tunawauzia umoja wa mataifa wakasaidie makambi ya wakimbizi. Watu wanalima na wanavuna.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie pia Tanzania ni miongoni mwa nchi tano (5) za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.
 
Kama ni lazima sana uwaambie, waambie waje wawekeze Tanzania, hakuna tena Rushwa, hakuna tena “ten percent” mambo yamenyooka.
 
Namalizia kwakushangaa leo watu waliochukua madini yetu, waliotutawala na kuwafanya watu weusi kuwa watumwa leo unawaomba wakuunge mkono ili uwe Rais, utakuwa Rais wetu au wa watu weupe, tutakua tumekuchangua sisi au umechaguliwa na wazungu. Hivi unapitishwa na wazungu kugombea Uraisi au na wanachama wa chama chako? Ni vikao vingapi vya chama haujahudhuria?
 
Mbaya Zaidi unajua mwenyekiti wa chama ambaye kimsingi ndiye aliyekupigania kutafuta fedha, kukaa na wewe Nairobi na kuja mpaka Ubeligiji umeamua kumwacha ateseke  na kutumia nafasi yako ya Urais ustaafu TLS kuwashawishi Mawakili wajitoe Ili aendelee kuteseka huku wewe ukitumia fursa hii kutafuta uraisi. Hauangaiki wala hata haufikirii kwamba ni wakati muafaka kurudi kuja kumpa moyo kama ambavyo alifanya yeye.
 
Kweli hayo ndio malipo unayompa Mbowe kwa kukuangaikia wewe upate matibabu bora. Tulitegemea wewe kama mwanasheria ungekuwa umerejea nchini na kumsaidia mbowe lakini uroho wa madaraka umekufanya kutumia matatizo yake kujiimarisha kisiasa na kutafuta uraisi.
 
Ni mimi Mdogo wako Paul Makonda.


from MPEKUZI http://bit.ly/2FLiwIV
via Malunde
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger