Wakati Rais John Magufuli akieleza sababu zinazomzuia kukutana na wanasiasa, viongozi wa vyama vya upinzani wamemtaka asiwe na hofu kukutana nao na kwamba pengine mtu aliyetishia kumchinja, alikuwa na maana ya “kuchinjwa kisiasa”.
Akizungumzia ushauri uliotolewa na Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la FGBF kutaka wanasiasa wakutane kama walivyofanya viongozi wa kidini, Rais alisema amekuwa akisita kwa sababu baadhi ya wanasiasa wanamtukana na wengine wametishia kumchinja na kumtupa baharini ndio maana ameamua awaache peke yao.
Hata hivyo, alisema yuko tayari kukutana nao.
Hayo yalitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300, ambako viongozi kadhaa wa kidini walipewa nafasi ya kufanya sala, akiwemo Askofu Kakobe, ambaye kabla ya sala aliomba aseme neno.
“Nimeusikia wito wa Mzee Kakobe kuwa walipokutana na wao (viongozi wa dini) kule, basi na sisi wanasiasa tuwe tunakutana,” alisema Rais.
“Mimi nimekubali sana, lakini tatizo ni kuwa huwezi kukutana na mtu anayekutana na kukuambia siku uchinjwe, utupwe baharini. Je, siku ukikutana naye iwe ndiyo siku ya kuchinjwa?”
Kauli hiyo ilimfanya mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda aombe radhi kama kiongozi wa wadau wa siasa na kwa niaba ya vyama vyote iwapo kuna kauli zimewahi kutolewa zenye mbomoko wa maadili.
“Nampongeza kwa kutambulisha utashi wake wa kutaka kukutana na viongozi wa vyama vya siasa. Hivyo kama kuna kauli ambayo imewahi kumkwaza atusamehe sisi wadau wa siasa kama ambavyo amekuwa akisamehe wafungwa ili na sisi tutoke kifungoni. Adhabu ya miaka mitatu inatosha,” alisema.
Alisema Rais anapaswa kuwapangia fursa ya kukutana nao ili awaeleze hisia zake na wao waeleze zao ili kudumisha utamaduni mzuri wa siasa kwa kuwa Tanzania ina deni la kuwa kielelezo cha siasa bora ya demokrasia ya vyama vingi.
Rais hakumtaja mtu aliyetoa tishio hilo la kuchinja, lakini wanasiasa wengi waliotoa lugha iliyotafsiriwa kuwa haifai, wamefikishwa mahakamani na baadhi kama mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi wameshatumikia adhabu ya kifungo.
Naye mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alisema bado msimamo wake ni meza ya mazungumzo na kwamba hata alipokutana na Rais Ikulu, Novemba 13 mwaka jana alimsisitiza jambo hilo.
“Kauli ya mtu mmoja asiichukulie vibaya. Anatakiwa kujua kuwa yeye ni jalala,” alisema mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi akirejea msemo maarufu wa “ukubwa ni jalala”.
“Awe na moyo wa uvumilivu, aweke kipaumbele cha taifa mbele kwa kuwa nchi ni kubwa zaidi ya mtu yeyote.”
Alisema Watanzania wote wanapaswa kutunza nguzo ya hekima, umoja na amani kwa kuwa jamii yoyote yenye migogoro haiwezi kustawi.
Mbatia alitoa mfano wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga ambao siku za hivi karibuni walishikana mikono kumaliza tofauti zao na wamekuwa wakionekana pamoja katika shughuli za kitaifa, kijamii na kiserikali.
Mbatia anaungwa mkono na kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alisema Rais Magufuli hakupaswa kutoa kauli kama hiyo ya “kuchinjwa na kutupwa baharini” kwa kuwa ana cheo cha Rais na amiri jeshi mkuu, lakini akasisitiza kuwa wamekuwa wakiomba kukutana naye kwa mwaka wa pili sasa.
“TCD wamemuandikia barua ya kutaka kuonana naye huu ni mwaka wa pili, lakini majibu yake ndio kama hayo unayoyaona. Hata juzi Mwenyekiti Mbatia alisema kuwa alipokutana naye alimkumbusha,” alisema Zitto
Naye naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salumu Mwalimu alisema kauli ya Rais Magufuli ilikuwa na utata kwa kuwa hakueleza ni kuchinjana kwa namna gani wala ni nani aliyewahi kuahidi kumchinja.
“Kuna vyama vya upinzani 18 yeye hajasema nani anataka kumchinja. Kama kuchinjana kisiasa ni sawa tu kwa kuwa tafsiri yake ni kuchuana, lakini kama ni kuchinjana kwa tafsiri nyingine sio kauli nzuri ina utata ndani yake maana kuchinjana si Utanzania,” alisema Mwalimu.
Kuhusu suala la kukutana na Rais Magufuili, Mwalimu alisema ustaarabu wa siasa ni pamoja na viongozi wa vyama kukutana na kujadili pamoja mambo ya kitaifa, kukosoana kwa heshima na kuruhusu hoja mbadala na hicho ndicho kimekuwa kikifanywa na viongozi waliopita, ndiyo maana siasa za taifa hili zimekuwa zikisifika.
“Siasa zetu zinapaswa kuwa upinzani na ushindani kama ilivyo kwa Simba na Yanga na si uadui. Tukiwa katika majukwaa tunachuana lakini tukishuka chini tunakunywa chai pamoja.
“Tunaoleana na tunashirikishana na kushauriana katika mambo mbalimbali wakati wa tatizo na wakati wa amani. Jambo hilo linarekebisha tabia hata za wafuasi wetu,” alisema Mwalimu.
Alisema Chadema haijawahi kuombwa kukutana na Rais ikakataa, wala haijawahi kusema haitaki kuonana na Rais. Alisema chama hicho kimekuwa kikikutana na marais wote hata Rais aliyepita walikutana naye mara kadhaa kwa kuwa alikuwa na siasa za kistaarabu.
“Hapa nchini kuna Rais mmoja tu, naye ana nafasi ya kutoa mwelekeo wa siasa za nchi. Kama kweli anataka kukutana na viongozi wa siasa ajiamini, aseme wala asiogope.”
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment