Mwanafunzi Hope Mwaibanje (18), aliyeibuka kinara katika Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) uliofanyika mwaka jana, ameeleza siri ya ufaulu wake.
Matokeo ya mtihani huo yalitangazwa jana jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, huku Mwaibanje akitangazwa kuwabwaga watahiniwa wenzake 322,964.
Akizungumza na Nipashe jana akiwa jijini Mbeya muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mwaibanje alieleza jinsi ilivyokuwa ngumu kwake kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 walioongoza kitaifa.
Alisema mara kwa mara walimu wao walikuwa wakiwaeleza kuwa, wakiweka juhudi katika masomo, watafanya vizuri kitaifa, ikizingatiwa shule yao (Ilboru) inasifika kwa kufanya vizuri na kutoa wanafunzi bora kitaifa mara kwa mara.
“Maneno haya ya walimu ndiyo yaliyonifikisha hapa nilipo, ingawa matarajio yangu hayakuwa haya, nilikuwa napambana niwe miongoni mwa wanafunzi 10 bora kitaifa, lakini Mungu ameamua kuniinua zaidi, namshukuru sana,” alisema.
Mwanafunzi huyo alisema ndoto yake ni kuwa daktari wa magonjwa ya moyo, anayoona ni changamoto kubwa nchini kwa sasa.
"Niseme ukweli, sikutegemea kama ningeongoza kitaifa, nilichokuwa napambana kusoma sana ni kuhakikisha kwenye wanafunzi 10 bora kitaifa sikosi, namshukuru Mungu, yeye ameamua kuniinua zaidi na kunifanya niongoze kitaifa,” alisema.
“Ratiba ya kuingia darasani ilikuwa inaanzia saa moja asubuhi hadi saa nane mchana, baada ya kutoka darasani kuanzia saa tisa alasiri hadi saa 12 jioni, nilikuwa najisomea mwenyewe. Baada ya hapo dini, tukimaliza kuanzia saa mbili usiku hadi saa sita nilikuwa najisomea.
“Niseme ukweli kutoka moyoni, walimu wetu pia walikuwa karibu na wanafunzi, walikuwa wanatufuatilia hatua kwa hatua za ufaulu wetu. Pia ninamshukuru Mungu kwa kuwa hakuniacha kila hatua.
“Endapo mwanafunzi akiamua kuachana na mambo mengine na kufikiria yale tu ambayo yamewapeleka masomoni, kwanini basi mwanafunzi wa namna hii asifikie lengo lake la kupata ufaulu wa juu, ila wasimwache Mungu."
Kinara huyo wa ufaulu alibainisha kuwa, kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, akiwa Shule ya Msingi Lioto, Mbeya Mjini, alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu bora, lakini alikutana na wakali zaidi alipojiunga na Ilboru na changamoto kubwa kwake ilikuwa lugha ya Kiingereza.
“Si unajua, unapotoka shule za msingi za serikali, lugha ya Kiingereza huwa changamoto, lakini hili halikunifanya nirudi nyuma, mwaka wa kwanza ulikuwa na changamoto na ufaulu wangu haukuwa mzuri, lakini kuanzia kidato cha pili nilifanya vizuri," alisema.
Mwaibanje alisema alipata taarifa ya kufanya vizuri kwenye mtihani huo jana asubuhi baada ya rafiki yake, Allen Diadoni kumpigia simu kumjulisha kuwa ameongoza kitaifa.
“Wakati huo nilikuwa nyumbani, sikuamini kwa sababu hayakuwa matarajio yangu, nikajua ananidanganya, lakini simu ziliendelea kupigwa za kupongezwa na baada ya muda nilihakikisha mwenyewe baada ya kuona matokeo yangu namshukuru Mungu," alisema.
0 comments:
Post a Comment