Saturday, 19 January 2019

Halmashauri 33 Zavuka Malengo Ya Ukusanyaji Wa Mapato

...
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Halmashauri 33  kati ya halmashauri 185 zimeweza kukusanya mapato ya ndani kwa kiwango cha asilimia 50 na zaidi ya makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 huku  halmashauri 21 zikiwa zimefanya vibaya kwa kusanya chini ya asilimi 20 ya makisio yake kwa mwaka.



Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo alipokuwa  akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa robo ya pili ya mwaka.

Alisema katika Halmashauri 33 zilizokusanya asilimia 50 na zaidi zimo Halmashauri za  Majiji tatu zikiongozwa na Jiji la Dodoma, Manispaa ni mbili zikiongozwa na manispaa ya Iringa, Halmashauri za Miji nane zikizongozwa na Mji wa Geita na Halmashauri za Wilaya ni ishirini zikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

“Uchambuzi unaonyesha kuwa Katika Majiji 6, Jiji la Dodoma linaongoza kwa kukusanya asilimia 59 ya makisio na Jiji la Tanga limekuwa la mwisho kwa kukusanya asilimia 33 ya makisio” alisema.

Aidha Manispaa ya Iringa imeongoza katika kundi la Manispaa kwa kukusanya asilimia 64 ya makisio ambapo Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 20 ya makisio.

Jafo aliongeza kuwa kwa upande wa Halmashauri za Miji, Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 84 ya makisio na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 9 tu ya makisio,

Alisema Katika kundi la Halmashauri za Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 78 ya makisio ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 6 tu ya makisio.

Kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ya mapato ya  Halmashauri Jafo alibainisha Halmashauri iliyoongoza kwa kuwa ni Jiji la Dodoma ambalo limekusanya Shilingi Bilioni 40.12 na halmashauri iliyokusanya kiasi kidogo cha fedha ni halmashauri ya Wilaya ya Momba ambayo imekusanya shilingi milioni 105.04.

Waziri Jafo pia alibainisha Mkoa ambao Halmashauri zake zimekusanya mapato kwa kuzingatia wingi wa mapato kuwa ni Mkoa wa Dar es salaam ambao kwa jumla halmashauri zake zimekusanya shilingi bilioni 77.4 na Mkoa wa Mwisho ni Katavi ambao halmashauri zake zimekusanya shilingi bilioni 2.4 tu.

Alisema katika Mkoa uliokusanya vizuri kwa kuzingatia asilimia ya makusanyo ni  Mkoa wa Geita Halmashauri zake zimekusanya asilimia 56.4 ya makisio ya mwaka ukifuatiwa kwa karibu na Mkoa wa Dodoma uliokusanya asilimia 55.9 ya makisio yake na Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Mtwara ambao umekusanya asilimia 15 ya makisio yake ya mwaka.

Wakati huo huo Waziri Jafo amewataka wakurugenzi wote ambao Halmashauri zao hazikufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya chini ya asilimia kumi ya makisio yake kwa kipindi cha nusu mwaka kujieleza na kujitathimini na kuhakikisha wanaongeza bidii katika suala la ukusanyaji wa mapato.

“Halmashauri 9 kati ya 10 zilizofanya vibaya katika mwaka wa fedha uliopita zimefanikiwa kufanya vizuri katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2018/19 kwa kukusanya zaidi ya asilimia 20 ya makisio yake” alisema .

Waziri Jafo pia aliwaagiza Wakurugenzi wote kuhakikisha takwimu zote za mapato katika mfumo wa LGRCIS zinafanyiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa IFMS(Epicor)  kwani taarifa zote za mapato na matumizi ya fedha zinatakiwa kutolewa kupitia mfumo huo.

Ulinganifu huu wa taarifa za mapato umelenga kuonesha jinsi kazi za ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa inavyoendelea kusimamiwa vyema na takwimu hizi zinazotolewa ni kwa mujibu wa taarifa zilizofanywiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa IFMS(Epicor).

Katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashaurti zilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na hadi kufikia Disemba 31,2018 Halmashauri zimekusanya shilingi bilioni 300 sawa na asilimia 41 ya makisio.

Kwa kipindi cha kwa mwaka 2017/18 halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 687.3 na hadi  kufikia Disemba,2017 halmashauri hizo zilikuwa zimekusanya sh bilioni 281.3 sawa na asilimia 41 ya makisio.

Takwimu hizi zinabainisha kuwa kuna ongezeko la Shilingi bilioni 18.7 kwa mwaka wa fedha 2018/19 ikilinganishwa na makusanyo kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger