David de Gea huenda akajijengea hadhi ya kuwa mlinda lango bora zaidi kuwahi kuichezea klabu ya Manchester United hasa baada ya ustadi wake Jumapili, kwa mujibu wa kaimu meneja wao Ole Gunnar Solskjaer.
Mhispania huyo mwenye miaka, 28, aliokoa mipira 11 na kuwawezesha United kuwalaza Tottenham 1-0 katika mechi iliyochezewa uwnaja wa Wembley.
Kwa mujibu wa BBC, katika miaka 11 aliyokuwa Old Trafford akiwa mshambuliaji, Solskjaer alicheza na magolikipa stadi kama vile Edwin van der Sar na Peter Schmeichel.
"Tumekuwa na magolikipa wazuri sana katika klabu hii na nafikiri kwa sasa anawatishia wote wawili Edwin na Peter katika nafasi hiyo ya kipa bora zaidi [kuwahi kuchezea United] katika historia," Solskjaer alisema.
De Gea aliokoa mipira 11 langoni katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya England na pia akawawezesha kumaliza mechi hiyo bila kufungwa.
Ushindi wao uliwawezesha United sasa kukamilisha ushindi wa mechi sita kati ya sita walizocheza chini ya Solskjaer.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania alijiunga na United kutoka Atletico Madrid mwaka 2011 na ameshinda tuzo ya mchezaji bora klabu wa mwaka katika misimu minne kati ya mitano ya karibuni zaidi.
"Alifaa kudaka mipira kadha," Solskjaer alitania.
"Tulikuwa na mabeki wazuri na David nyuma yao mambo yalikwenda vyema ajabu. Unaruhusiwa kuwa na kipa mzuri.
"Nimecheza na magolikipa kadha wazuri sana. Tumekuwa na utamaduni wa kuwa nao na amekomaa na kukomaa hata zaidi. Alistahiki tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mechi ya leo (jana)."
Solskjaer ameshinda mechi tano za ligi mfululizo akiwa na United matokeo ambayo sasa yamewawezesha kutua nafasi ya sita wakiwa sawa kwa alama na Arsneal walio nafasi ya tano, wakiwa mbele kwa wingi wa mabao.
United wamo alama sita pekee kutoka nafasi ya nne inayowezesha klabu kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
"Bado tunaamini kwamba tunaweza kumaliza katika nne bora," alisema De Gea.
"Sisi ni United, tuna wachezaji wazuri na tunang'ang'ania kumaliza katika nne bora.
"Ilikuwa mechi nzuri sana, hata zaidi ukizingatia tulikuwa uwanja wa Wembley. Zilikuwa alama tatu muhimu sana. Ninafurahia sana uchezaji wangu na timu inacheza vyema sana pia, na kuunda nafasi na kucheza soka ya kushambulia zaidi.
"Tumecheza mechi tatu sasa mtawalia bila kufungwa, jambo ambalo ni zuri sana. Wachezaji wana furaha, na unaweza kuliona hilo uwanjani, wanachezaji wa kujituma sana, kama Manchester United."
0 comments:
Post a Comment