Tuesday 15 April 2014

BUNGENI LEO DODOMA 15/04/2014

...


April 15, 2014, Muungano bado kasheshe
Kikao cha Bunge maalum la katiba kinaendelea leo hii, kinachojadiliwa hasa ni sura ya kwanza na sita ya Rasimu ya Katiba.
Kama ilivyo kawaida, wajumbe wanaendelea kulumbana, Chama Cha Mapinduzi wakikazania Muundo wa serikali mbili na wale wa upinzani wakitetea serikali tatu, kama ilivyowasilishwa na Tume Maalum ya kukusanya maoni iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Wajumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, ambao ni muhimu sana kwa ajili ya upatikanaji wa Katiba hii, kwa kuwa ni lazima theluthi mbili wakubali ili kupitisha kipengele chochote, wanaendelea kuvutana, juu ya serikali mbili au tatu huku pia wakipigana vijembe.
Zifuatazo ni baadhi ya kauli zilizosisimua kutoka kwa baadhi ya wajumbe

Mh. Mbaruku: Anaunga muundo wa serikali mbili maana ndiyo anaamini utawapa Zanzibar utajiri na Zanzibar itakuwa Half London.

Mh. Hija Hassan Hija: Anasema watanganyika hawana hasara ya serikali mbili wala moja maana walishachukua mali zote kwa miaka 50 iliyopita na Zanzibar wameibiwa kwa miaka 50 iliyopita. Zanzibar ilipwe kwa muda huo.
Anasema wenye mali ni Tanganyika, mawaziri wa Zanzibar wamekuwa wakisema muungano umekuwa ukiwaonea na anashangaa ni nini kimewapata. Anasema kuna mawaziri wana maslahi yao ndo maana wanashindwa kuipigania Zanzibar.
Anasema hawatetei muungano bali wanatetea maslahi yao maana kuna watu walikuwa wanapigania muungano ila baada ya kupewa uwaziri wakakaa kimya kwa hiyo hawa ni wasaka tonge, wana njaa.

 Mh. Pamela Masai: Anasema wajumbe wameacha maslahi yenye tija kwa watanzania wote na kukimbilia kwenye muundo wa serikali.
Anaunga mkono maoni ya wachache kwenye Kamati namba 10. Na anaunga mkono Lugha ya kiswahili kutumika kama lugha ya taifa.
Anapinga vipengele vya Uadilifu, uwajibikaji uwazi na usawa kuondoshwa kweye tunu ya taifa.
Anasema kamati zote zimeunga mkono sura ya pili ibara ya sita 2(6), anasema kwa hiyo hata mamlaka waliyonayo wajumbe wa BMK ni mamlaka waliyopewa wananchi.
Anapendekeza muundo wa Serikali tatu. Anasema kama wananchi wanataka serikali mbili basi waendelee na serikali tatu alafu wananchi wapendekeze maoni ya muundo wa serikali wanayotaka.

Mh. Mwinyi Haji Makame: Anasema muungano huu waasisi wetu wameleta muungano wa undugu na sio vinginevyo.
Gari ya serikali mbili ishachemka na haizuiliki, anasema hata wakina Jussa wakileta unafiki na chuki muundo huu utaendelea kuwepo..
Anasema miaka 50 ya Mapinduzi ndiyo umeijenga Zanzibar.
Anamalizia kwa kusema kuwa matatizo ya Zanzibar kwa muundo huu wa serikali mbili yashashughulikiwa ndani ya kamati zote zilizoundwa kutatua matatizo ya wazanzibar.

Mh. Chiku Abwao: Anaanza kwa kusema yeye ni muumini wa muungano na muungano wa shirikisho ndiyo utaondoa muungano wa manung'uniko na kuhakikisha Tanganyika inapatikana kwa gharama yoyote, ananukuu ''Jasiri ni yule anayejali kwao''
Anasema bora muungano uvunjike ila Tanganyika ibaki na anaunga muundo uliopendekezwa na tume ya Warioba maana ni maoni ya wananchi walio wengi.
Anamnukuu Lukuvi kuhusu jeshi kutawala nchi kama muundo wa serikali tatu ukipita na kusema hata hivyo jeshi lipo kwa ajili ya wananchi wa Tanzania pia anawasifu wazanzibar kwa kupigania utaifa wao.
Anasema wabunge walio wengi wa tanzania hawapo bungeni kuunga muungano wa tanganyika na zanzibar bali wapo kuunga mkono muungano wa TANU na AFRO-SHIRAZI Party.

Mh. Oluoch: Anasema kumbe bungeni ni sehemu ambapo ukweli unaachwa na uongo kuchukuliwa. Anasema hata waasisi waliunganisha mchanga wa Tanganyika na Zanzibar ili kuunda serikali moja na sio mbili kama ilivyo sasa.
Anasema ikiwa wazanzibar wakitaka muungano hawatapiga kura ya kuunga muundo wa serikali mbili...
Anasema walimu wanaunga hoja serikali tatu.

Shamsa Mwangunga: Anatoa pongezi kwa serikali ya JMT kwa kulea muungano huu mpaka kufikia miaka 50 maana malezi yanapitia changamoto nyingi.
Anasema muungano huu ni tunu maana nchi nyingi zimejaribu kuwa na muungano na shirikisho ila hawakuweza kufika mbali ila kwa muungano huu wa Tanzania ni suala la kujivunia kuwepo mpaka sasa hivi. Uvumilivu na upendo wa watanzania ndo umeleta muungano huu kuwa imara na kero mbali mbali zimeweza kutatuliwa na kubaki kero moja ya uchumi.
Utawala bora tumekuwa tukisifiwa duniani kwa kuwa na utawala bora kwa kuweza kuudumisha muungano huu na kuna watu wamekuwa wakipotosha kuwa kuna kero wakati sio kweli hakuna kero na kero zilizobaki ni ndogo na zinafanyiwa kazi.
Anasema serikali ya nchi mbili ni zimwi tulijualo na tumelizoe na serikali ya nchi tatu hatulijui ''Zimwi likujualo halikuli likakwishaaaa''

Mh. Salehe Nassoro Juma: Msimamo wake ni muungano wa serikali tatu na anawatoa wasiwasi watanzania na wapemba wanaofanya biashara ya vitunguu tanzania bara kuwa serikali tatu hazivunji muungano na kama ukivunjika tanzania imesaini mkataka wa haki za binadamu na wataendelea kuishi kama DIASPORA hata muungano ukivunjika.
Anamshukuru mh. Kikwete kwa kuanzisha mchakato huu wa katiba mpya, maana kabla ya mchakato huu ilikuwa kosa la jinai kuzungumzia muundo wa muungano.
Anasema hakuna asiyejua kuwa muundo wa serikali mbili una tatizo na suluhisho la matatizo haya ni muundo wa serikali tatu, anasema pia kuwa mawazo ya waasisi wetu yamezeeka inabidi yafanyiwe modification na ametolea mfano wa China jinsi walivyofanyia modification mawazo ya waasisi wao na mambo yanaenda vizuri.

Mh. Haji Omar: Anaanza kwa kuunga mawazo aliyoyatoa kwenye kamati no 7 mawazo ya walio wengi kwenye sura ya 1 & 6 juu ya muundo wa serikali mbili.
Uhalai wa Karume kuchukua dhamana ya watu wa Zanzibar kuhusu muungano, anasema mzee Karume alikuwa anatimiza ilani ya chama chake cha ASP juu ya umoja na kuhakikisha elimu, matibabu yanakuwa bure na makazi bora kwa wazanzibar wote.
Faida za muungano, anasema
1.Umeme jimbo la Tumbatu
2. -Anasema wananchi walio wengi Zanzibar wanaunga muundo wa serikali mbili.

Mh. Ezekiel Maige: Anasema kuwa lugha zinazotolewa na Wazanzibari zina ukakasi. Anasema kuwa Zanzibar ina wilaya 10 ambazo zote zina barabara za lami na umeme tofauti na Tanzania Bara.
Anasema kuwa hayo yote hawayaoni na badala yake wanazidi kulalamika kuwa wanaonewa na Bara. Anahoji iwapo ikatokea Zanzibar kukawa na utajiri mkubwa kuliko Bara, je Wazanzibari watakuwa tayari kuisaidia Bara?

Mh. Fahmi Dovutwa: Alama za taifa zitakua wimbo wa taifa, nembo ya taifa na bendera. Dola haimtambui Mungu kwa hiyo wimbo wa taifa itolewe kwenye alama ya taifa. dhana ya kuomba Mungu asaidie ina maana dola haifungamani na dini. Nami ntasimama nitapigana kuhakikisha Katiba inamtambua Mungu.
Kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine. Sera ya TANU iliruhusu wazee watoto na walemavu kunyonya. Nataka iwe kutegemeana sio kunyonyana.
Watu wanaoamini serikali tatu mpaka sasa wameshindwa kutuonesha jinsi watakavyotatua matatizo tulio nayo. watu wa serikali tatu wameshindwa kujenga hoja. Namlaumu sana Mbowe. Chadema wana serikali za majimbo lakini wanashindwa kufafanua vizuri.
Natoa shukrani za pekee za Rais kwa kuridhia hii ijadiliwe na kusimamia elimu za kata. Namshukuru pia Lowasa aliye mshauri Rais.

Mh. Joseph Mbilinyi: Naunga mkono serikali tatu kama ilivyoletwa na Tume ya katiba, kwa hiyo tunaunga mkono maoni ya wananchi.
Aliyeharibu huu mchakato ni Rais aliyekuja kuelezea msimamo wa chama chake badala ya kuzindua bunge.
Hiki ni kipindi cha Kwaresma acheni unafiki. Tumeharibu pesa nyingi. CCM wameishiwa mikakati wameanzisha mkakati wa kuzomea. Mwingulu anataka serikali moja lakini anaogopa kusema. Tuko kwenye nafasi nzuri sana la kujadili hili suala la sivyo tutalijadili kwa kulazimishwa.

Leo Lukuvi anatutishia nchi itatawaliwa na jeshi, vizuri, mbona Rais wetu alikua mwanajeshi na anatuongoza? wanajeshi ni ndugu zetu, wakitawala kuna tatizo gani?

Serikali tatu ni tija. kila chenye gharama kina faida. Mara nyingi viongozi wa dini wanakosea wanapokuwa upande wa dola dhidi ya wananchi. Mfano Rwanda. Unapopima malaria au ukimwi inapimwa kwenye kidole sio mwili mzima acheni kuzingua eti waliohojiwa ni wachache.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger