Na Hudugu Ng'amilo
RAIS
Jakaya Kikwete amehujumiwa na viongozi wakuu wastaafu waliomlazimisha
kuachana na msimamo wa muundo wa muungano wa serikali tatu na kukumbatia
serikali mbili zilizopendekezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa
kutoka kwa baadhi ya vyanzo vya habari vilivyo karibu na rais, Ikulu na
makao makuu ya CCM, zimelithibitishia kwamba hadi Bunge Maalumu la
Katiba linaanza, Rais Kikwete alikuwa na msimamo ule ule wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Baadhi
ya viongozi wastaafu, wakiwamo marais na viongozi waandamizi wa CCM,
walishinikiza rais aachane na serikali tatu, kwa vitisho kwamba zitaua
muungano.
Baadhi
ya wastaafu hao walimficha Rais Kikwete kwamba kwa kuwa yeye aliingia
madarakani akiwa rais wa muungano wa serikali mbili, halikuwa jambo la
busara kwake kujiingiza kwenye historia ya kuwa rais aliyevunja
muungano.
Kwa
mujibu wa vyanzo vyetu, shinikizo hilo liliambatana na jingine la
kumtaka asizindue Bunge kabla ya rasimu ya pili ya katiba mpya
kuwasilishwa bungeni, ili apate fursa ya kudhoofisha hoja ya serikali
tatu.
Mara
baada ya Rais Kikwete kukubaliana na "washauri wake", serikali
ililazimika kuingilia kati ili Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta atengue
kanuni, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba awasilishe rasimu kabla
ya rais kuzindua Bunge, jambo ambalo limesababisha mvurugano unaotishia
kuvuruga kabisa mchakato wa katiba mpya.
Hata
hivyo, hali hiyo inasemekana kumnyima amani Rais Kikwete ambaye ndiye
aliyepokea na kusaini rasimu hiyo, kwa maana kwamba aliridhia.
Uamuzi huo umefanya rais aonekane kiongozi asiye na msimamo thabiti katika masuala muhimu.
Baadhi
ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai hatua hii imemfanya
ashindwe kuacha urithi makini na muhimu katika utawala wake wa miaka 10,
kama ambavyo alikuwa amedhamiria.
Wadadisi
wanasema wastaafu walimzuia rais kutekeleza azima yake kwa sababu ya
hofu tu, wakidhani kwamba katiba mpya yenye mfumo mpya inaweza kufumua
mambo yaliyofichika na kuwaingiza matatani.
Wanadai
kwamba muungano wenye mfumo mpya una kila dalili za kuiondoa CCM
madarakani, na kuhatarisha maslahi ya watawala waliopo na waliopita.
Hoja hii, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, ndiyo ilimkuna Rais Kikwete hata akabadili msimamo.
Kwa hali halisi ilivyo, na mchakato unavyoendelea, ahadi ya Rais Kikwete kuwapa Watanzania katiba mpya mwezi huu imeshindikana.
Alipohutubia
taifa na kutangaza kuanzisha mchakato wa katiba mpya miaka mitatu
iliyopita, alisema kwamba lengo lake lilikuwa kuzindua katiba mpya
katika maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya muungano iliyofanyika jana.
Hadi
Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa juzi, zilikuwa zimepita siku 68
kati ya 70 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, huku kukiwapo
mgawanyiko mkubwa wa wajumbe na kutishia uhai wa muungano, hasa baada ya
wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia Bunge
baada ya kukerwa na hujuma na matusi kutoka kwa wajumbe wenzao wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Hadi
sasa Bunge la Katiba limefanikiwa kujadili sura mbili za rasimu bila ya
kuzipigia kura. CCM imekataa maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
yanayopendekeza mfumo wa muungano wa serikali tatu, wakatetea mfumo wa
serikali mbili.
Mapendekezo
hayo ni kinyume kabisa cha yaliyomo kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyowasilishwa ili ijadiliwe na wajumbe hao na kisha kutunga
katiba mpya.
UKAWA
wanadai kuchoshwa na vitisho na matusi kutoka kwa wajumbe wa CCM na
viongozi wa serikali, wakisema kuwa kwa hali ilivyo katiba bora ya
wananchi haiwezi kupatikana kwa shinikizo la muundo wa serikali mbili.
Katika
hili, Rais Kikwete analalamikiwa kuwa ndiye mvurugaji wa kwanza wa
mchakato ambao aliuasisi na kuahidi kuwapatia wananchi katiba bora kabla
ya kuondoka madarakani.
Wakati
akilihutubia Bunge la Katiba na kulizindua rasmi Machi mwaka huu, Rais
Kikwete aliibeza rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, akisema takwimu zao
kuhusu watu waliotoa maoni ya muundo wa muungano zinatiliwa shaka.
Alisema
kuwa muundo wa serikali tatu unaopendekezwa hautekelezeki kwani rais wa
dola hiyo hatakuwa na mamlaka kwa vile hana ardhi, rasilimali na hivyo
hataweza kukopa.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, katika hali kama hiyo, jeshi linaweza kupindua
serikali na hivyo ukawa mwanzo wa kuvunjika kwa muungano, huku
akisisitiza kwamba wao kama CCM muundo ambao unaweza kutatua kero
zilizopo ni ule wa sasa wa serikali mbili.
Kauli
hiyo ya rais iliibua mjadala mkubwa, na hivyo kufifisha ndoto za
kupatikana kwa katiba bora kwani ilionyesha wazi kwamba mapendekezo ya
wananchi ya serikali tatu yaliyomo kwenye rasimu hayatazingatiwa.
Hali
hiyo imeendelea kujitokeza kwenye Bunge Maalumu la Katiba baada ya
wajumbe wote wa CCM kuendeleza msimamo wa rais wa serikali mbili na
kumshambulia Jaji Warioba binafsi kwa matusi mazito wakidai ana ajenda
ya kuvunja muungano kwa kupendekeza serikali tatu.
Hatua
ya Rais Kikwete kubadilika na kuvuruga mchakato aliyouasisi na
kuusimamia kwa mafanikio makubwa, imeelezwa kusababishwa na mambo
makubwa mawili, likiwemo hilo la kuburuzwa na viongozi wastaafu.
Duru
nyingine za kisiasa katika suala hilo la kukwama kwa mchakato wa
katiba, zinahusisha na rasilimali ya gesi na mafuta zilizopatikana
nchini, ambapo inadaiwa mataifa makubwa yanayotaka kuwekeza ndiyo
yanaishinikiza serikali isibadili muundo wa muungano uliopo.
Vyanzo
vyetu vya habari vinaeleza kwamba mataifa hayo tayari yameweka msimamo
wa kuisaidia CCM kifedha ili kuhakikisha inapigana kufa au kupona
kutobadili muundo wa muungano katika katiba mpya.
Inaelezwa
kuwa muundo wa shirikisho la serikali tatu unaopendekezwa kwenye rasimu
ya katiba mpya, unatoa fursa ya wazi kwa wananchi wa serikali washirika
kusimamia rasilimali zao tofauti na ilivyo katika muundo wa sasa ambapo
mambo mengi yamefanywa siri na serikali.
Hadi
sasa majaliwa ya kupatikana kwa katiba mpya yametoweka baada ya UKAWA
kujiondoa, na hivyo kulifanya Bunge la Katiba kushindwa kufanya maamuzi
ya kupitisha ibara na sura za rasimu kutokana na theluthi mbili ya
wajumbe kutoka Zanzibar kushindikana.
Chanzo Tanzania Daima.
Chanzo Tanzania Daima.
0 comments:
Post a Comment