Mfanyabiashara
Yusuph Manji jana alitii sheria bila shuruti kwa kuhama kwenye jengo la
Quality Plaza akitekeleza amri ya Mahakama ya kumtaka kurejesha jengo
hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Mbali
na kutekeleza amri ya kuhama baada ya kupewa notisi ya saa 24
iliyomalizika juzi, pia anatakiwa kulipa malimbikizo ya deni la pango la
Dola za Marekani 6.1 milioni (zaidi ya Sh13 bilioni), ambazo kama
asipozilipa mali zake zitakamatwa.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Mahakama Kitengo cha Ardhi kutoa hukumu ya
kumtaka Manji kuondoka kwenye jengo hilo pamoja na kuilipa deni la
pango.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.
Viongozi
wa kampuni za Manji waliokuwa wakisimamia uondoaji wa vifaa
uliomalizika jana asubuhi, walikataa kuzungumza na waandishi wa habari
waliofika kufuatilia tukio hilo.
Tangu
juzi chini ya usimamizi wa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart,
Manji na kampuni zake walikuwa wanaondoa vifaa mbalimbali vilivyopo
kwenye jengo hilo na kuhitimisha shughuli hiyo jana.
Meneja
Uendeshaji wa Yono Auction Mart, Atukuzwe Mhugo alisema kampuni ambazo
walikuwa wakizisimamia kuondoa vifaa ni Quality Group Co Ltd, Gaming
Managemeti Ltd, Q Consult Ltd na Quality Logistics Co Ltd.
Hata
hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya Yono, Scholastica Kenyela
alisema tayari wameshaziondoa kampuni za Manji kwenye jengo hilo.
Kenyela
alisema mteja wao ambaye ni PSPF alichukua uamuzi huo baada ya Manji
kushindwa kulipa kodi ya pango ya zaidi ya Sh13 bilioni.
“Sisi
tumetimiza wajibu wetu, ukienda pale utaona tayari tumeshafanya kazi
yetu kwa sababu alipewa notisi ya saa 24 awe ameondoka,” alisema.
Ofisa
Uhusiano Mwandamizi wa PSPF, Abdul Njaidi alisema masuala yote
yanayohusiana na jengo hilo kwa sasa yako chini ya Yono Auction Mart. “Sipo Dar es Salaam na sitazung- umzia chochote kuhusu jengo hilo wenye mamlaka ni Yono naomba uwatafute wao,” alisema.
0 comments:
Post a Comment