Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ baada ya
kudaiwa kumfanyia fujo jirani yake ameendelea kujibu madai hayo kwa
mtindo wa ‘kudonoa donoa’ na jana aliwataka wanaodai kuwa alilewa siku
hiyo wataje alikunywa pombe gani na katika baa gani.
Wiki
mbili zilizopita, taarifa kwenye vyombo vya habari zilisema kwamba
Mchungaji Lusekelo alikwaruzana na majirani zake huku akidaiwa kuwa
alikuwa amelewa jambo ambalo lilifanya achukuliwe na kuhojiwa na
polisi.
Lakini,
tangu kuibuka kwa tukio hilo alikataa kulitolea ufafanuzi licha ya
kutafutwa na vyombo vya habari, hata pale alipohudhuria ibada kanisani
kwake aliwaambia waumini wake hatalizungumzia na badala yake
alidonoadonoa baadhi ya matukio.
Alipokwenda
kanisa kwake kwa mara ya kwanza Novemba 25, Mchungaji Lusekelo alisema;
“Kuna kitu nilikuwa nataka nikiseme, lakini sitakisema ili waendelee
kusema haohao waliokuwa wanasema.Wakawaulize wenyewe. Nimeyaona magazeti
hapa, ooh Mzee wa Upako, ooh Mzee wa Upako, sisemi. Sasa leo yupo hapa,
na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda. Hii ni kama
kumpiga chura teke.”
Lakini,
Novemba 28, Mchungaji huyo akajibu baadhi ya hoja akisema kwanza,
maneno aliyotumia ambayo ni mshenzi, mpumbavu na mjinga siyo matusi
kwani yameandikwa kwenye Biblia. Pili, watu hao ndiyo walianza kumtukana
yeye baada ya kuwauliza wanatafuta nini eneo la getini kwake.
Hoja
nyingine alisema watu hao hawakuwa jirani zake kama inavyodaiwa kwani
mtaani kwake wanaishi kama majambazi kutokana na mazingira ya
kutofahamiana.
Jana,
Mchungaji Lusekelo akiwahubiria waumini wake alidonoa tena eneo jingine
linalohusiana na tukio hilo, kwamba wanaodai alikuwa amelewa pombe,
waeleze alikunywa pombe gani na baa gani.
Akikaribishwa
kwa wimbo wa kuabudu uitwao, ‘Nina haja nawe’ kabla ya kuanza kumtunza
kwa sadaka, Mchungaji Lusekelo alisema watu wanaotuhumu kuwa alilewa,
wanatakiwa kueleza alikunywa pombe gani na alikunywa akiwa eneo gani.
“Wiki
iliyopita nilikuwa Wizara ya Mambo ya Ndani, baadhi ya maofisa
wakaniona , wewe Mzee wa Upako… Mzee wa Upako, askari mmoja akaniuliza
wewe Mzee wa Upako unachukua sadaka halafu unaenda kunywa pombe.
Nikawauliza, hiyo pombe nilikunywa wapi, halafu pombe zipo za aina
nyingi, taja ni pombe gani, ukienda mbali zaidi ungeuliza nililewa nini,
maana hata upako wa roho mtakatifu ni ulevi,” alisema.
“Lakini
kuna majina ya watu, mitaani inaitwa pombe, sasa sijui ni pombe gani
hiyo….watashindana sana. Lakini kushindana siyo tatizo, je, mtashinda?
Eti oooh hayo maneno tu hata kwenye kanga yapo, subiri tusiandikie mate
na wino upo, ukitaka kummaliza Mzee wa Upako we mpige risasi tu,”
alisema huku akishangiliwa na waumini wake.
Alisema hakuna mwanadamu atakayeweza kumwangusha kwa kipawa na kalama Mungu aliyompatia.
“Ndiyo
maana unapojiita mtume leo unakuwa unajirusha kwenye harakati ambazo
zilijengwa na baba zetu, ndiyo maana kumshinda shetani ni lazima, kuna
mfumo umejengwa na mfumo huu uko imara kama chuma cha pua,” alisema.
Katika
ibada ya wiki iliyopita, mchungaji huyo alisema taarifa zinazosambazwa
kumchafua hazitamvunja moyo wa kuendelea kufanya kazi ya uchungaji, huku
akihoji kwanini magazeti yanaandika mabaya pekee na hayaandiki habari
za uponyaji anaofanya kanisani kwake.
0 comments:
Post a Comment