WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa kila Mtanzania na haitamvumilia mtu wala kikundi chochote kitakachofanya mambo yanayotishia usalama na amani ya nchi.
Aidha, ametaka migogoro katika nyumba za ibada, ikiwemo misikiti imalizwe ndani kwa kutumia mabaraza badala ya kutoka nje kwa jamii kwani inaashiria sura mbaya ya kiimani na haina tija.
Majaliwa aliyasema hayo jana alipozungumza katika Baraza la Maulid ya kumbukizi ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba, mkoani Singida na kurushwa hewani na televisheni ya TBC1.
Maulid ilisomwa juzi usiku na mapumziko pamoja na Baraza la Maulid ilikuwa jana.
Kabla ya kuzungumzia ujumbe huo kuhusu amani ya nchi, Majaliwa alimshukuru Rais John Magufuli kwa kusitisha kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) isiendelee hadi jana ili kumwezesha kuhudhuria Baraza hilo la Maulid.
Waziri Mkuu alisema serikali haitayumba katika kusimamia usalama wa nchi na kuhakikisha hakuna nafasi kwa kikundi chochote kitakachoipeleka nchi pabaya na kuwataka viongozi wa dini kuwahakikisha waumini wao hawaenezi chuki dhidi ya imani nyingine.
“Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kila mwananchi kuabudu kile anachoona kinafaa. Serikali itafanya kila liwezekanalo kusimamia na kuhakikisha hakuna kikundi kinahatarisha usalama wa nchi na hatutayumba katika hilo,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mara nyingi huwa napenda kurejea kauli ya Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliyosema kuwa: Nchi haina dini bali watu wake wana dini, na kusimamia hilo kwamba tutaendelea kuwezesha uhuru wa kuabudu.”
Hata hivyo, alionya kuwa pamoja na serikali kusimamia uhuru wa kuabudu, haitawavumilia watakaotoa mahubiri yasiyozingatia misingi ya sheria na kanuni za nchi na yenye kumuumiza mtu wa imani nyingine.
Pamoja na hayo, alisema mpaka sasa dini zote nchini zinafanya vizuri katika kuhubiri imani zao na amani ya nchi, jambo linaloendelea kuifanya Tanzania kuwa kimbilio kwa wananchi wa mataifa yenye mapigano. “Bado Tanzania imeendelea kuwa kimbilio kwa wanaopigana, sisi hatuna mahali pa kwenda, kama wao wanakuja hapa kwetu sisi tutakwenda wapi? Ukitafakari hilo utadumisha amani,” alisema Majaliwa.
Akijibu risala iliyosomwa kwake ikielezea mambo kadhaa ikiwemo tishio la ugaidi, watu kubambikiziwa kesi kwa chuki, kuundwa kwa kamati ya kitaifa ya Kiislamu kushughulikia maadili na uanzishwaji wa chombo cha maarifa (Daruu/Nyumba ya Maarifa), Waziri Mkuu alisema ni masuala ambayo serikali inayachukulia kwa uzito wake.
Alisema serikali inatambua uwepo wa matishio ya ugaidi sehemu mbalimbali na pamoja na kwamba ipo imara, inahitaji nguvu ya pamoja ya wananchi kukabiliana na vitendo hivyo na matendo maovu yote.
Kuhusu migogoro katika nyumba za ibada, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kumekuwa na ugomvi na migogoro katika maeneo ya ibada ya watu kugombea madaraka na uongozi na kuleta taswira mbaya.
Akielezea upande wa misikiti, majaliwa alisema ugomvi na migogoro katika misikiti ni sura mbaya, haina tija na inapaswa kumalizwa ndani na si kutoka nje.
“Tutumie mabaraza yetu kutatua migogoro ndani ya misikiti yetu,” alieleza na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kutegemea dini kuimarisha amani nchini, na kuwataka pia waumini wa dini hiyo na viongozi kutokukaa bila kufanya kazi kwani hata vitabu vingine vya Mungu ikiwemo Biblia Takatifu, vinaeleza wazi kuwa, asiyefanya kazi na asile.
Waziri Mkuu pia alizungumzia kuhusu uwajibikaji wa watumishi wa umma na kusema kuwa hatua ambazo serikali inachukua kwa watumishi wake ni sahihi na kamwe haitarudi nyuma katika kusimamia haki za Watanzania bila kujali dini, rangi wala kabila.
Alizungumzia pia suala la maadili kwa vijana na jamii kwa ujumla na kutaka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwalea vijana katika malezi ya kiislamu kwa ajili ya kuwaandaa kuwa viongozi wema wa sasa na baadaye kwa dini na taifa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwatakia Wakristo kote nchini sikukuu njema ya kuzaliwa Yesu Kristo Desemba 25 na pia aliwatakia Watanzania wote sherehe njema za kuupokea Mwaka Mpya 2017.
Kauli ya Mwigulu Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza katika baraza hilo, alisema wizara yake inasimamia taasisi zote za kiimani na kutaka viongozi wa dini wasaidie kuwafichua wanaofanya uovu kwa kisingizio cha dini.
Alisema mtu akifanya kosa asihukumiwe kwa dini au imani yake, bali liwe kosa la mtu husika ili kuendelea kuifanya nchi kuwa ya dini mbalimbali na yenye uhuru wa kuabudu.
“Ikitokea Idd hata kule bungeni huwa tunashiriki, hii suti si ya jana, hivyo tusaidiane kuwafichua wanaofanya uovu na kusababisha makosa, lawama na taswira ziende kwenye taasisi zilizotukuka na taasisi tukufu,” alisema Mwigulu.
Aidha, alitoa mabati 1,500 mwaka juzi na mwaka huu kwa ajili ya misikiti iliyofikia hatua ya kupauliwa na kama bado ipo kwenye misingi, aliahidi kutoa saruji.
Pia alisema alikutana na viongozi wa Kiislamu mjini Dodoma na kuzungumza suala la usafiri na kuahidi kuwapatia gari kwa shughuli za Bakwata wilayani Iramba. “Sasa niwaambie jambo hilo limekamilika baada ya wiki mbili tumeni dereva tumepata Noah kwa ajili ya Bakwata yetu ya wilaya ya Iramba,” alieleza Mwigulu.
Mufti ahimiza amani, furaha Kwa upande wake, Mufti Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeiri alisema kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na maisha yake kwa ujumla yalilenga furaha, amani na umoja wa kuishi kindugu baina ya Waislamu, wasio waislamu na jamii nzima.
Mufti alitaka Waislamu wamuenzi Mtume Muhammad kwa kuacha majungu, fitina na kuishi kwa upendo.
“Umma huu siku hizi kila mtu shehe, si kweli, na si kila shehe anafaa, anayefaa si shehe wa fitina, asiyejua neno gani aliseme wapi, kwenye harusi anatia neno la msiba,” alisema Mufti akizungumzia viongozi kujitathimini kauli zao na kutii mamlaka zilizopo madarakani kwa kuwa kila zama zina namna yake ya uongozi.
Akizungumzia uchumi, aliagiza viongozi wa Kiislamu kufanya kazi badala ya kujificha katika imani akisisitiza mtu akikaa tu bila kazi hapaswi kulalamika hana kitu.
“Mbingu hainyeshi mvua ya dhahabu wala ya fedha, ukiweka mikono juu, Mungu nipe nipe, akupeje umekaa tu,” alieleza. “Fanya kazi usiduseduse tu katika majumba ya watu, unasalimia, fanyakazi acha kula vyakula vya watu kwa kigezo cha kumcha Mungu,” alisema Mufti.
Aliitaka misikiti na madrasa ianzishe vyanzo vya mapato kuepuka kutegemea wafadhili ili kupata mashehe wazuri wenye elimu ya dini na ya dunia badala ya kujingamba kuwa wewe si mtu wa mchezo kumbe hakuna lolote.
0 comments:
Post a Comment