Tuesday, 13 December 2016

CCM Dimani yapitisha 3 mchujo wa awali ubunge

...

 
WAGOMBEA watatu wa nafasi ya kinyang’anyiro cha ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani Zanzibar, wamepitishwa katika hatua ya awali na mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo hilo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Magharibi, Yahya Saleh alithibitisha kupitishwa kwa majina hayo, ambayo yatapelekwa mbele ya Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa ajili ya uchambuzi zaidi na kupigiwa kura.
Majina ya wanachama waliopitishwa kugombea nafasi ya ubunge Dimani katika hatua ya tatu bora ni Juma Ali Juma, Hussein Migoda Mataka pamoja na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Hafidh Ali Tahir ambaye nafasi yake ilichukuwa katika uchaguzi wa mwaka jana, Abdalla Sheria.
“Tumepitisha majina matatu ya wagombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Dimani katika hatua ya awali na majina hayo yatapelekwa mbele ya Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa uchambuzi zaidi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi kichama, Yussuf Mohamed aliwataka viongozi kujenga mshikamano huku wakiweka mbele mikakati na malengo ya kuhakikisha chama cha Mapinduzi kinashinda katika uchaguzi huo.
Alisema wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu wana sifa na vigezo vya kuongoza, lakini katika utaratibu wa awali lazima wapungue ili kupata idadi inayohitajika na hatimaye mtu mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo.
“Tulikuwa na wagombea 16, lakini sasa tunao watatu ambao tutakwenda na hatimaye kupata jina la mtu mmoja tu ambaye ndiye atakayepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi huo,” alieleza mweneyekiti huyo.
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani utafanyika Januari 22, mwakani, kujaza nafasi ya Hafidh Ali Tahir aliyefariki ghafla mkoani Dodoma mwezi uliopita wakati akihudhuria vikao vya Bunge.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger