WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa mambo ya malikale na
uhifadhi wa urithi asilia (natural heritage) watafute mbinu
zitakazoimarisha utunzaji wa rasilmali hizo bila kuathiri mifumo ya
uchumi ya nchi zinazoendelea.
Ametoa
wito huo jana (Jumanne, Mei 31, 2016), wakati akifungua Mkutano wa
Kimataifa wa siku nne unaojadili Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika
kama Nyenzo ya kuleta Maendeleo Endelevu ulioanza leo kwenye ukumbi wa
mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Waziri
Mkuu alisema kuna baadhi ya nchi ambazo ni maskini sana lakini
zimebarikiwa kuwa na rasilmali kama madini na gesi asilia lakini kwa
sababu rasilmali hizo ziko karibu sana na vivutio vya urithi asilia wa
dunia, watu wa nchi hizo wanazuiwa kuchuma rasilmali zao ili wasiharibu
vivutio hivyo.
“Tunatambua
umuhimu wa kutunza rasilmali na vivutio vya urithi asilia. Hivi ni kwa
nini zisitafutwe teknolojia zinazofaa ambazo zitaruhusu uvunaji wa gesi
asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wa vivutio vya urithi asilia wa
dunia (world heritage sites)?”, alihoji Waziri Mkuu.
“Serikali
za nchi za Kiafrika zinahitaji suluhisho kama hili wakati zikiendelea
kutafuta njia sahihi za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya urithi wa
dunia na changamoto ya kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” amesema.
“Sisi
viongozi ambao wengi wetu ni wanasiasa, hatukatai ushauri wa wataalamu
lakini tunawasihi baadhi yenu ambao mnashiriki mkutano huu muhimu,
mtafute njia mbadala za kufumbua tatizo hili badala ya kuendelea
kutegemea njia za kizamani za kukabiliana na changamoto kama hizi ili
sote tuweze kunufaika na rasilmali zilizopo ikiwa ni pamoja na kutunza
vivutio vya urithi asilia wa dunia,” aliongeza.
Alisema
kama rasilmali hizo zitachambuliwa vizuri na kwa njia sahihi bila
kuathiri vivutio vya urithi wa dunia, ni dhahiri kuwa zitaingiza mapato
ambayo kiuchumi yatasaidia kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi ambao
pia watasaidia kwenye uhifadhi wa vivutio hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu
alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilmali nyingi zikiwemo za
ardhini (madini), misitu, wanyama na maeneo ya kihistoria na kusisitiza
kuwa Watanzania wana jukumu la kuzilinda ili zilete tija kwa wananchi
wote.
“Tukizitunza
rasilmali zetu zitasaidia kupata mapato kutokana na utalii Serikali
itapeleka sehemu ya mapato haya katika miradi mbalimbali na hivyo
kuchangia kwenye pato la Taifa,” amesema.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe
amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na UNESCO hasa katika masuala
yanayohusu uhifadhi wa vivutio vya dunia kutokana na umuhimu wake kwenye
maendeleo endelevu.
Alisema
wizara yake imelenga kusimamia, kuendeleza na kuimarisha utunzaji wa
maliasili na uhifadhi wa vivutio asilia na vya kiutamaduni (natural and
cultural heritage) kwa kushirikiana na wadau wengine hapa nchini.
Naye
Mkurugenzi wa Uhifadhi Malikale wa UNESCO, Dk. Mechtild Rossler
aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali duniani wawe
tayari kupitia upya shughuli zinazotekelezwa katika eneo la urithi wa
dunia na kuangalia wajibu wa nchi za Kiafrika katika kuandaa mwelekeo wa
miaka ijayo.
Alisema
katika miaka 40 ya utendaji wa UNESCO, idadi ya vivutio vya urithi wa
dunia imeongezeka na kufikia 89 ambapo kati ya hivyo viko baadhi
vinakavyobiliwa na changamoto ya kufutika kutokana na athari za kigaidi,
matukio ya kivita na kazi za kibinadamu.
“Vivutio
16 kati ya 48 viko katika nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la
Sahara na hivi vinakabiliwa na tishio la kupotea kutokana na vita,
harakati za kigaidi na shughuli za kiuchumi za kibinadamu zikiwemo
uchimbaji wa madini na gesi asilia,” alisema.
Aliwataka
washiriki wa mkutano huo wakumbuke kuwa vivutio vya urithi wa dunia ni
vielelezo vya jamii na pia huchangia uchumi kwa kutoa ajira kwenye jamii
husika.
Mkutano
huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 kutoka nchi mbalimbali
duniani, unajumuisha washiriki kutoka nchi 36 zikiwemo nchi 12 ambazo ni
za nje ya bara la Afrika.
Waziri Mkuu amerejea mjini Dodoma jana mchana kuendelea na vikao vya Bunge.
0 comments:
Post a Comment