Serikali inatarajia kutangaza nafasi mpya za ajira za walimu mara baada ya bajeti kuu ya serikali kupitishwa na Bunge.
Katibu mkuu wa wizara ya Tamisemi Mhandisi Musa Iyombe aliyasema hayo
jana jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu uzushi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa serikali
imesitisha ajira za walimu wa masomo ya sanaa na biashara.
Alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba kinachosubiriwa ili
kutangazwa kwa ajira hizo ni Bajeti kuu kupitishwa na Bunge. Bajeti kuu
ya serikali itapitishwa na kuanza kutumika rasmi Julai 1.
"Tumesikitishwa na taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii,
kuwa tamisemi imesitisha ajira za walimu. Tamisemi inapenda kuujulisha
umma kuwa taarifa hiyo ni batili na inalenga kuchonganisha wananchi na
serikali yao ya awamu hii" Alisema.
Alisema pia taarifa hiyo imelenga kuwapa hofu na chuki walimu waliohitimu masomo ya sanaa na biashara.
Iyombe alisema utaratibu utakaotumika kutangaza nafasi za ajira kwa
walimu haujabadirika na kwamba utatumika uliozoeeleka miaka yote.
Sambamba na hilo, alitaka wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano,
kuwasaka na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kusambaza taarifa
hizo za uongo.
"Tamisemi inaitaka Mamlaka yenye dhamana ya kusimamia mitandao ya
kijamii ichunguze na kubain aliyesambaza taarifa hizi za uongo na
achukuliwe hatua stahiki" alisema
Kwa upande wake katibu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini,
Profesa faustini Kamuzora, alisema kuna sheria ya mtandao ambayo
itatumika ili kuhakikisha watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Taarifa hiyo iliyokuwa imesambazwa mitandaoni ilieleza kuwa serikali
inatarajia kuajiri masomo ya Hisabati na Sayansi pekee na kwamba walimu
wa masomo ya Sanaa na Biashara hawataajiriwa.
0 comments:
Post a Comment