Imeelezwa kuwa idadi ya wanyamapori aina ya Faru weusi[Black Rhino] imepungua kutoka faru zaidi ya elfu kumi kwa miaka 1970 mpaka 1980 na kubaki faru 161 pekee hadi sasa hapa nchini kutokana na Ujangili.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Dokta Hamis Kigwangalla wakati akizindua mpango kazi wa kulinda na kutunza Faru weusi uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Dokta Kigwangalla amesema kutokana na tishio kubwa la faru kutoweka hapa nchini kwa sababu ya ujangili, serikali imeandaa mikakati kabambe ya kudhibiti ujangili hali ambayo imeanza kuzaa matunda na kuanza kusababisha faru kuongezeka ambapo serikali imetenga Dola milioni 61 sawa na zaidi ya Tsh.Bilioni 120 za kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.
Aidha,Dokta Kigwangalla amesema sekta ya utalii hapa nchini huzalisha zaidi ya Dola za Marekani bilioni 2 ambazo huchangia asilimia 25% ya fedha za kigeni na kuchangia asilimia 17% ya mapato ya ndani ya nchi [GDP ] na imetoa ajira rasmi laki sita[600,000] na zisizo rasmi milioni mbili[2000,000] hivyo ulinzi wa wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka wakiwemo faru utaendelea kuimarishwa na mpango wa serikali ni kuhakikisha uzalishaji wa faru unaongezeka kwa kasi kwa miaka mitano ijayo.
Katika hatua nyingine ,Dokta Kigwangalla ameitaka jamii kuachana na mila potofu za kutumia pembe za faru kama dawa za kuongeza nguvu za kiume kwani imani hizo hazina ukweli wowote na zinapaswa kupuuzwa.
Mtafiti kutoka taasisi ya utafiti ya wanyamapori nchini,TAWIRI Dokta Edward Kohi amesema kunahitaji teknolojia zaidi ili kuhakikisha faru anatunzwa ambapo miaka ya 1998 waliingia kwenye tatizo la kutoweka hadi sasa kuna faru 161 wanaoweza kuhesabiwa na kuonekana.
Pia ,Dokta Kohi ametaja malengo madhubuti ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania,[TAWIRI ] ni Pamoja kuongeza idadi ya faru si chini ya 5% kwa mwaka,kuwa na uwezo wa kuhamisha faru kutoka eneo moja hadi jingine,kuhakikisha ujangili wa faru uwe chini ya 1% pamoja na kuwa na mfumo wa mawasiliano na mipaka mingine.
Naye mwakilishi kutoka mfuko wa wanyamapori ulimwenguni[WWF] Dokta Simon Lugandu amesema mradi wa kuhifadhi na kutunza faru Tanzania unaendelea katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ‘
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilishaanza kutumia teknolojia ya kufuatilia faru ambapo mradi wa teknolojia hiyo ya kifaa chenye uwezo wa kutoa maelezo mwenendo wa faru ,unagharimu dola za kimarekani 111,320 na unatekelezwa kwa ushirikiano na maafisa wa TANAPA ,Maafisa wa Shirika la Wanyama la Frankfurt[FZS]na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania[TAWIRI]
0 comments:
Post a Comment