Friday 19 July 2019

Serikali Kuanza kusajili nyaraka za ardhi ndani ya mkoa husika badala ya utaratibu wa mwanzo wa kusajiliwa ndani ya kanda

...
Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, amesema serikali itaanza kusajili nyaraka za ardhi ndani ya mkoa husika, badala ya utaratibu wa mwanzo  wa kusajiliwa ndani ya kanda zilizokuwa zimetengwa.
 
Waziri Lukuvi amesema  lengo ni kupunguza ucheleweshaji wa usajili wa nyaraka hizo na kuepusha usumbufu kwa wananchi.

Waziri Lukuvi ametoa kauli hiyo leo   Julai 18,2019 Jijini Dodoma wakati akifungua, mkutano wa wataalamu wa sekta ya ardhi, wanaokutana jijini  Dodoma, kutathmini wapi walipo na malengo ya sekta hiyo, sambamba na kuwaje uwezo wataalamu  hao namna bora ya ufanyaji  kazi na namna ya kutatua changamoto zilizopo.
 
Amesema wamekusudia kuhamisha ofisi za kusajili nyaraka za ardhi kutoka katika kanda, na kuzirudisha ndani ya mikoa husika, ili kurahisisha zoezi hilo, na upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati,  na tayari wakuu wa mikoa wameridhia na kutoa majengo yatakayotumika kama ofisi za wizara za usajili ndani  ya mikoa.
 
“Serikali imeamua kuunda ofisi za ardhi ngazi ya mkoa  na sio kanda kama ilivyokuwa awali.
 
Hii ni kupunguza gharama ,hivyo michoro yote ya ardhi sasa inapitishwa mkoani,taarifa za uthamini wa ardhi  ambazo zilikuwa zinapatikana makao makuu sasa atateuliwa mthamini mkuu kila mkoa,Idara zote za ardhi zipangwe upya na wenye tabia za ovyo hawatapangwa”amesema.
 
Aidha Waziri Lukuvi amesema katika  kuhakikisha wananchi wanyonge wanapata huduma stahiki, amepiga marufuku wakuu wa idara za ardhi kupokea tozo ambazo hazistahili, pamoja na utumiaji wa madalali ndani ya ofisi za umma.
 
Amemtaka katibu mkuu wa wizara hiyo Doroth Mwanyika, kuhakikisha anapanga safu ya wakuu wa idara  haraka watakao kwenda kufanya kazi katika ofisi za wilaya na ofisi za mipango miji na orodha hiyo ipite mikononi mwake kabla ya wahusika kupewa barua za uteuzi.
 
Pia  Waziri Lukuvi ametoa maelekezo kwa maafisa  ardhi kutojihusisha na kampuni binafsi  za upimaji ,kutopokea au kutoza fedha  kinyume na taratibu katika upimaji wa ardhi,kutojihusisha na madalali wasiolipa kodi,kila wilaya kuhimiza kukusanya kodi,pamoja na kuwa na bei elekezi  katika upimaji wa ardhi.
 
“Tabia chafu ya kupokea na kuingiza  fedha bila utaratibu maalum Dodoma inafanyika sana,maafisa  ardhi mnawajua  matapeli lakini mnashirikiana nao ,Pia nawaagiza vibali vya ujenzi visitolewe zaidi ya  wiki moja na kwa viwango vilivyokubaliwa .Nimekuta baadhi ya halmashauri mtu anatozwa zaidi ya laki tano ili apate kibali cha ujenzi huu ni unyonyaji,Nitakula sahani moja na kila ,mtu ,bado kuna madudu mengi sana kwa watumishi wa ardhi   Double Location bado yapo”.amesema.
 
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amewasimamisha kazi  watumishi wa Ardhi ambao ni Manase Kastory aliyekuwa afisa ardhi Mikindani   Lindi na alihamishiwa Sengerema Mwanza ambapo waziri Lukuvi amesema afisa wa ardhi huyo  alifanya uhuni wa uchakachuaji wa michoro ya ardhi  Mikindani.
 
Maafisa ardhi wengine wanaochunguzwa ni afisa ardhi Rufiji,na afisa ardhi Kilwa aliyejulikana kwa jina moja la Sultan  ambaye amedhulumu Tsh.Mil.35 .
 
Kwa upande wake Katibu mkuu wa Wizara hiyo Doroth Mwanyika, amebainisha malengo ya kukutana katika mkutano huo.
 
Na kauli mbiu ya mkutano huo ni “Mabadiliko katika sekta ya ardhi kwa maendeleo ya taifa letu”.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger